Wananchi Malinyi walia kukosa huduma za afya

Wananchi wakiwa tayari kupokea msaada wa chakula kutoka kamati ya maafa ya Mkoa wa Morogoro baada ya kuathirika na mafuriko wilayani Malinyi. Picha na Johnson James

Muktasari:

  • Wakati mafuriko yakiwa yameikumba Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, wananchi wamelalamika kukosa huduma za afya na kupanda kwa bei ya bidhaa.

Morogoro. Pamoja na Serikali kutumia usafiri wa anga kutoa misaada ya chakula kwa waathirika wa mafuriko wilayani Kilombero na Malinyi mkoani hapa, wananchi wa Kata za Usangule na Misegese wameomba kupata suluhisho la kudumu la huduma za tiba.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 27, 2024 wakati wa kupokea misaada iliyoletwa na helikopta ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), baadhi ya wananchi wa Kata ya Misegese wamesema kwa sasa changamoto yao kubwa ni ukosefu wa tiba kwa kuwa hospitali hazifikiki.

Alphonce Geofrey mkazi wa Misegese amesema, “changamoto tunayopata vituo vya afya viko mbali na hapa tunapoishi na barabara zimekatika kutokana na mvua kubwa zinazonyesha, hivyo ikitokea mtu ameugua tunapata tabu kumfikisha kupata tiba, hivyo iko haja ya Serikali kutuangalia kwa jicho la karibu ili afya zetu ziwe salama.

"Kwenye kata yetu hii huwezi kutoka kwenda eneo jingine la jirani, maana maji bado yapo, barabara hazipitiki na hata ule usafiri wa bodaboda ambao tumekuwa tukiutumia kwa sasa haufanyi kazi vizuri," amesema.

Kwa upande wake Anitha Charles ameiomba Serikali iendeleze usafiri huo wa anga kutoa huduma hasa za afya katika kipindi hiki cha mvua.

"Kwa kuwa Serikali imeamua kutumia usafiri wa anga kutupa msaada wa vyakula, nashauri walau wafanye mpango helikopta hiyo iwe na wataalamu wa afya wafanye kliniki hata mara tatu kwa wiki ili wagonjwa watakaopatikana kwenye eneo letu hili wapate matibabu," amesema.  

Naye Emmanuel Rashid mkazi wa Malinyi amesema mvua zikinyesha hospitali ya wilaya ya Malinyi huwa maji yanajaa mpaka usawa wa madirisha.

Diwani wa Kata ya Usangule, Fadhili Luguguda amesema kwenye kata yake maisha yamekuwa magumu kwa vitu kupanda bei kutokana na kukosekana  mawasiliano ya barabara.

"Jografia ya kata hii tupo kama kisiwani, ukitaka kwenda sehemu yoyote lazima utembee kwa miguu maana hata bodaboda kuna maeneo haziwezi kukatiza kutokana na wingi wa maji, hivyo hilo limesababisha maisha yanakuwa magumu kwa bidhaa kupanda bei.”

"Kiberiti cha Sh100, kwa sasa kinauzwa kati ya Sh400 hadi Sh500, sukari kilo moja inauzwa kati ya Sh7,000 hadi Sh8,000 hili ni ongezeko kubwa la vitu ambalo halijawahi kutokea,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba amesema ni kweli maeneo hayo yameathirika na mafuriko na Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha miundombinu inarejea kama kawaida.

"Kwenye wilaya yetu ni kweli maeneo hayo yameathirika na mafuriko kwa kiasi kikubwa, barabara zimeenda na maji na hata makaravati tuliyokuwa tunaamini yangetusaidia nayo yalizidiwa na wingi wa maji na kubomoka.”

“Lakini huduma muhimu zinaendelea kupatikana kwa hali tuliyonayo na sisi kama Serikali jicho letu liko karibu," amesema.