Mvua yasababisha DC wa Malinyi kushindwa kutumia ofisi kwa siku saba

Mkuu wa wilaya ya Malinyi Mathayo Maselle akiwa ndani ya Mtumbwi akiwa ameshika fedha akitoa kwa waliopatwa na mafuriko,majin ya Mvua yamejaa katika mji wa Malinyi na na kuleta Athari kwa taasisi za Serikali.

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mathayo Masele ameshindwa kutumia ofisi yake kwa siku saba mfululizo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo

Morogoro. Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mathayo Masele ameshindwa kutumia ofisi yake kwa siku saba mfululizo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo na kusababisha maji kujaa kwenye taasisi mbalimbali ikiwezo ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo, hospitali pamoja na shule za msingi na sekondari.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Jumatano, Machi 11, 2020, Masele amesema kwa sasa kazi zake amekuwa akifanya nje ya ofisi yake kwa kuwafikia wananchi mahali walipo pamoja kutokana na hali hiyo.
“Ni kweli jengo la mkuu wa wilaya limeingiliwa na maji na sio langu tu hata shule za msingi na sekondari, hospitali na kwa mkurugenzi, mimi nafanya kazi popote sio lazima niwe ofisini wananchi wanapata huduma kama kawaida,” amesema.
Masele amesema mvua zimekuwa zikinyesha mara kwa mara wilayani humo na kwa siku tatu zilizopita ilinyesha kuanzia saa 2 hadi 9 usiku na kusababisha maeneo mengi kuwa chepechepe jambo lililotokana na mto Fulua kujaa maji kwa sababu ya  mvua zinazonyesha katika wilaya jirani kama Mahenge na Ulanga.
Mmoja wananchi aliyezungumza na Mwananchi, Msonde Samson amesema watu wamepata madhara na baadhi yao kuhama nyumba zao kutokana na kujaa maji.
Ameiomba Serikali kuwasaidia katika kuhakikisha wanaweka miundombinu ya mji wa Malinyi katika hali bora huku akiupongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa namna unavyofanya jitihada za kutoa misaada mbalimbsali kwa walioathirika na mvua.