Wananchi Muheza mbaroni wakidaiwa kuchoma moto gari la ofisa kilimo

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Muheza linawashikilia wananchi kwa tuhuma ya kuchoma gari la ofisa kilimo, wakimtuhumu kushindwa kuwasimamia.

Muheza. Jeshi la Polisi wilaya ya Muheza mkoani Tanga, linawashikilia wananchi kadhaa wa kijiji cha Kambai kilichopo Kata ya Kwezitu kwa tuhuma ya kuchoma gari la ofisa kilimo wa kata ya Tongwe, ikiwemo kumjeruhi wakimtuhumu kushindwa kusimamia maslahi yao.

Inaelezwa wananchi wameibua hali hiyo baada ya kuibuka sintofahamu kutokana na ujio wa wawekezaji katika kijiji cha Kambai wilaya ya Muheza.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Abdallah, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Muheza (OCD), Hadija Sokolo amesema wanawashikilia wananchi hao kwa mahojiano kutokana na tukio la kuchomwa moto kwa ofisa huyo.

Amesema kwa sasa ofisa kilimo huyo amelazwa Hospitali ya Wilaya Muheza akipatiwa matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kishambuliwa na wananchi hao.

Amesema baada ya kupokea taarifa hizo amelazimika kufika katika kijiji hicho, ili kufanya mkutano na wananchi kwa lengo la kutafutia ufumbuzi suala hilo na kwamba ameunda timu maalumu ya watu 10 kuchunguza tukio hilo la wananchi kuchoma moto gari la ofisa kilimo huyo.

Mkuu huyo wa wilaya amesema Halmashauri ya Wilaya Muheza ina eneo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 3,000 lenye hati kwa zaidi ya miaka 28, lakini kwa miaka yote hiyo halijaendelezwa na ndipo mwaka 2020/2021 alipatikana mwekezaji na akapewa ekari 500.

Hata hivyo, inaelezwa alipewa eneo hilo bila kufanyika tathmini ya kina na mwaka jana walipatikana wawekezaji wengine wanne nao pia tathmini ya kina haikufanyika, hali ambayo imeleta sintofahamu kati ya wananchi  na halmshauri.

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Abdallah

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa mkuu wa wilaya ya Muheza,  Zainab,  mkuu wa Polisi wilaya (OCD) Muheza, Hadija Sokolo amesema wanawashikilia wananchi kadhaa kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo.

Tukio hilo linafanana na lililowahi kutokea mwaka 2016 katika kijiji cha Iringa, Mvumi wilayani Chamwino ambapo watafiti wanne wa masuala ya ardhi walishambuliwa na wananchi kwa mapanga na kuuawa, kisha gari walilokuwa nalo kuchomwa moto.

Mbali na kuuawa kwa watafiti hao kutoka Chuo cha Utafiti wa Udongo na Maendeleo ya Ardhi cha Selian mkoani Arusha, gari la Serikali aina ya Toyota Hillux Pick-Up lilichomwa moto na wananchi.