Wananchi Rungwe wapewa siku 60 kupisha ujenzi wa barabara

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya ,Jaffar Haniu akizungumza na wananchi.

Muktasari:

Mradi huo utatekelezwa na mkandarasi, kampuni ya China Road Constructions ambayo itakuwa kichocheo ya kufungua fursa za kiuchumi kwa wakulima kusafirisha mazao.

Mbeya. Wakati Serikali ikitoa zaidi ya Sh87 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, wananchi wametakiwa kuondoa mali zao kwenye hifadhi ya barabara ndani ya siku 60 ili kupisha ujenzi huo.

Barabara zitakazojengwa ni ya kutoka Katumba hadi Lupaso kilomita 35.5 na ya  Mbaka kwenda Kibanja, kilomita 20.7 ambapo imetajwa kuwa kichocheo cha shughuli za kiuchumi hususan usafirishaji wa mazao.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Mei 9, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu amesema tayari mkandarasi amefika kwa ajili ya kuanza utekelezaji.

Amesema wakati mradi huo ukianza kutekelezwa, wananchi wametakiwa kuondoa mali zao kwenye hifadhi ya barabara umbali wa mita 22.5 kwa hiari yao.

“Nimetoa siku 60 wananchi wawe wameondoka kupisha mradi huo ambao utakuwa na mafanikio makubwa katika kusafirisha mazao kama chai, parachichi, viazi mviringo na ndizi.”

“Unajua Rungwe wananchi wanajihusisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara, uwepo wa barabara utakwenda kuwa mwarobaini kwa wananchi ikizingatiwa kuna barabara zilikata mawasiliano kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha,” amesema Haniu.

Pia, amewasihi wananchi kujiepusha na vitendo vya uhalifu na badala yake wawe mstari wa mbele kuwafichua.

Wakati huohuo, Haniu ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kutoa ushirikiano kwa mkandarasi aliyepeta tenda sambamba na kutoa ajira kwa vijana wazawa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Halmashauri ya Busokelo, Anyosisye Njobelo ameishukuru Serikali kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo muhimu ambayo itafungua fursa za kiuchumi na kuchochea mapato.

Amesema mradi huo ukikamilika utakwenda kuondoa adha kwa wakulima kusafirisha mazao kwa gharama nafuu, tofauti na sasa ambapo ziko juu kwa sababu ya ubovu wa miundombinu.