Wananchi wachanga Sh40 milioni kujenga shule

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni akishiriki shughuli ya ujenzi wa Madarasa yanayojengwa kwa nguvu za wananchi katika Kijiji Cha Vuje. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Wananchi wa vijiji vya Iriama na Mgambo, Kata ya Vuje, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro wamechangishana fedha zaidi ya Sh40 milioni kuanzisha shule yao mpya ya sekondari kutokana na watoto wao kutembea zaidi ya kilomita 20 kwenda kwenye shule ya kata ambayo ipo umbali mrefu.

Same. Wananchi wa wa vijiji vya Iriama na Mgambo, Kata ya Vuje, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, wamechangishana fedha zaidi ya Sh40 milioni kuanzisha shule yao mpya ya Sekondari kutokana na watoto wao kutembea zaidi ya kilomita 20 kwenda kwenye shule ya kata ambayo ipo umbali mrefu.

Wananchi hao wamesema wataendelea kuchangishana fedha ili wanafunzi watakaochaguliwa kidato cha kwanza mwakani waweze kujiunga na shule hiyo huku wakiiomba Serikali kuongeza nguvu katika umaliziaji wa madarasa ya shule hiyo ambayo yapo katika hatua ya upauaji wa vyumba vinne vya madarasa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati Mkuu wa Wilaya hiyo, Kasilda Mgeni alipokwenda kutembelea mahali inapojengwa shule hiyo, wamesema watoto wao wamekuwa wakiamka usiku wa manane kwenda shule ya kata ambayo ipo umbali mrefu  hali ambayo wamesema inahatarisha usalama wa maisha ya watoto wao ikiwemo kukumbana na wanyama wakali.

Gudluck Sechuma, Mkazi wa Kijiji cha Vuje ambaye ni Mwenyekiti wa ujenzi wa shule hiyo, amesema walianza kujenga shule hiyo tangu mwaka 2008 kwa nguvu zao wenyewe baada ya kuona wanafunzi wanateseka kwa kuamka usiku wa manane kwenda shule lakini kutembea zaidi ya Kilomita 20 kwenda shule ya kata ambayo ipo mbali.

"Tumeamua kujenga shule hii ya pili katika kata yetu hii kutokana na kwamba wanafunzi wa Iriama na Mgambo wanatembea umbali mrefu zaidi ya kilomita 20 kila siku kutokana na shule iliyopo ya kata kuwa mbali na vijiji hivi,  hivyo wananchi wa kijiji hiki kwa pamoja tukaona kuna umuhimu wa kujenga shule hii ya pili katika kata yetu," amesema.

"Shule hii ilianza kujengwa mwaka 2008 kwa nguvu zetu kwa kupitia msaragambo na nguvu za vijana wetu ambao wapo maeneo mbalimbali, mpaka sasa tumepandisha madarasa yenye vyumba vinne na sasa madarasa mawili tayari tumepaua na mengine yanaendelea kupauliwa,  tunamshukuru mkuu wa wilaya kwa kuungana nasi na tunaamini Januari ikifika wanafunzi wa kidato cha kwanza wataanzia hapa," amesema.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho,  Navoneiwa Mchome,  amesema kukamilika kwa majengo hayo wanafunzi watapata unafuu kwa kuwa muda mwingi  wanautumia barabarani na hata wanapofika shuleni wanakuwa wamechoka na hivyo kunaweza kuchochoa ufauli mbaya kwa wanafunzi.

"Kilichofanya tujenge shule hii ni  kutokana na watoto wetu kutoka usiku wa manane kwenda shule ya sekondari Kenga ambayo ipo mbali sana, watoto wanatoka usiku wa manane na njiani wanakumbana na changamoto nyingi hasa kwa watoto wetu wa kike, " amesema.

"Tunaomba serikali iweke mkono wake ili hawa watoto wetu wasipate tabu ya kutembea umbali mrefu tena maana kwa watoto wa kike ni hatari sana, tunatamani hawa wanaoanza kidato cha kwanza mwakani waingie hapa," amesema.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Kasilda Mgeni amesema serikali kwa kuona mchango mkubwa wa wananchi hao katika kuiunga mkono serikali yao atahakikisha anashirikiana na halmashauri kuona namna ya kuongeza nguvu katika umaliziaji wa shule hiyo.

"Lazima serikali tuone namna ya kuwaunga mkono wananchi hawa waliojitolea kwa nguvu zao wenyewe,  mara kadhaa tumekuwa tukihimiza wananchi watumie nguvu zao na sisi tutakuja kumalizia,  sasa wananchi wameonyesha njia, tutaona ni namna gani ya kuwatia nguvu hawa wananchi, ni hatua kubwa mmefanya," amesema.

"Tunapona wananchi wanaendelea na moyo wa kujitolea kwenye maeneo yetu sisi kama serikali tunawaunga mkono ili ule moyo uendelee, serikali imeona nguvu zenu na mimi hapa nitakwenda kuongea na Mkurugenzi wa Halmashauri tuone chakufanya  ili tuwatie moyo," amesema.

Hata hivyo mkuu huyo wa Wilaya amesema ofisi yake itatoa kiasi kidogo cha fedha kuungana na wananchi hao kutokana na juhudi kubwa walizoonyesha na kuwataka kuendelea kuwa na mshikamani huo.