Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi waelimisha uoteshaji miti kisasa kukabili mabadiliko ya tabianchi

Wananchi na Watumishi wa Sao Hill wakiendelea na zoezi la upandaji miti katika Shamba la hilo la miti  lililopo Wilayani Mufindi mkoani Iringa. Picha na mtandao

Muktasari:

  • Shughuli hiyo imefanyika kwa kuchukua miche ya miti katika shamba la miti Sao Hill lengo likiwa ni kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira na wananchi wanaoishi jirani na shamba hilo wakinufaika kiuchumi na kielimu kupitia ushiriki wao katika zoezi hilo.

Iringa. Wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka Shamba la Miti Sao Hill Wilayani Mufindi mkoani Iringa wameendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchukuaji na upandaji wa miche ya miti, hatua inayochangia moja kwa moja juhudi za kulinda mazingira na kuendeleza rasilimali za misitu nchini.

Ushiriki wa wananchi katika shughuli hizo umeongeza nguvu katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, huku ukihimiza matumizi endelevu ya misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Zoezi hilo limefanyika leo Januari 15, 2026 ambapo shughuli za uchukuaji miche ya miti zimeendelea kwa ufanisi katika bustani za miche zilizopo Tarafa ya Kwanza Irundi na Tarafa ya Tatu Ihalimba ndani ya Shamba la Miti Sao Hill.

Mmoja wa wananchi walioshiriki zoezi hilo, Joshua Ng’umbi kutoka Kijiji cha Igowole Wilaya ya Mufindi, amesema kuwa ushiriki wake umemsaidia kupata kipato pamoja na ujuzi mpya.

Ng'umbi amesema kuwa amejifunza namna ya kuchagua miche bora na kupanda miti kwa njia sahihi ili iweze kukua vizuri na kutoa faida kiuchumi wakati wa uvunaji.

Wananchi na Watumishi wa Sao Hill wakiendelea na zoezi la upandaji miti katika Shamba la hilo la miti  lililopo Wilayani Mufindi mkoani Iringa. Picha na Mtandao

Aidha shughuli hizo ni sehemu ya mwendelezo wa upandaji miti unaotekelezwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa lengo la kuendeleza misitu ya kupandwa, kuongeza uzalishaji wa rasilimali za misitu na kuhakikisha uendelevu wa uhifadhi wa mazingira.

Kupitia zoezi hilo, wananchi kutoka maeneo yanayozunguka shamba hilo wamepata fursa ya ajira za muda, hali iliyowawezesha kuongeza kipato na kuboresha maisha yao ya kila siku.

Mbali na kunufaika kiuchumi, wananchi wanaoshiriki wamepata elimu ya vitendo kuhusu namna bora ya kuanzisha na kusimamia bustani za miche ya miti kwa kuzingatia kanuni za kitaalamu.

Katika hatua nyingine Wananchi hao wamejifunza hatua mbalimbali za uzalishaji wa miche ikiwemo upandaji wa mbegu, utunzaji wa miche, umwagiliaji sahihi pamoja na maandalizi ya miche kabla ya kupandwa shambani.

Kupitia zoezi hilo, wananchi pia wamepata uelewa wa mbinu bora za upandaji miti mashambani ikiwemo nafasi sahihi kati ya mti na mti pamoja na muda mwafaka wa kupanda.

Elimu hiyo imewawezesha wananchi kuelewa umuhimu wa matunzo ya awali ya miti baada ya kupandwa ili kuhakikisha inakua vizuri na kuchangia uhifadhi wa mazingira kwa muda mrefu.

Shughuli za uchukuaji na upandaji miche zimeongeza uelewa wa wananchi kuhusu mchango wa Shamba la Miti Sao Hill katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali za misitu.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Said Singano, amesema kuwa uchukuaji wa miche unafanyika kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya kitaalamu.

Wananchi na Watumishi wa Sao Hill wakiendelea na zoezi la upandaji miti katika Shamba la hilo la miti  lililopo Wilayani Mufindi mkoani Iringa. Picha na Mtandao

"Hii miche huchukuliwa kwa uangalifu mkubwa ili kulinda mizizi yake, kwa kuwa ubora wa miche ni msingi muhimu wa mafanikio ya upandaji miti mashambani," amesema PCO Singano

Kwa mujibu wa PCO Singano ameeleza kuwa miche yenye ubora mzuri huongeza nafasi ya miti kuota vizuri, kukua kwa afya na kutoa mazao bora ya misitu kwa matumizi ya baadaye.

Vilevile uchukuaji miche Shamba la Miti Sao Hill zimeendelea kuwa chachu ya uhifadhi wa mazingira, kutoa ajira kwa wananchi na kuimarisha ushirikiano kati ya TFS na jamii inayozunguka shamba hilo.