Mara wapanda miti milioni saba
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akipanda mti katika Shule ya Msingi Buhare Kati Manispaa ya Musoma ikiwa ni sehemu ya kampeni ya mkoa huo kupanda miti milioni 13 kwa mwaka 2026. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Zaidi ya miti milioni saba imepandwa mkoani Mara katika kipindi cha mwaka 2025 huku mkoa huo ukilenga kupanda miti milioni 13 lengo kuu likiwa ni kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Musoma. Zaidi ya miti milioni saba imepandwa mkoani Mara katika kipindi cha mwaka 2025 huku lengo pamoja na mambo mengine likiwa ni kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambazo zimeanza kujitokeza katika maeneo mbalimbali nchini ikiwepo mkoani Mara.
Takwimu hizo zimetolewa mjini Musoma leo Jumatano Januari 14,2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi wakati wa upandaji miti kupitia kampeni ya mti wa Mama, 27 ya kijani kampeni iliyoandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
Hata hivyo Kanali Mtambi hakuweza kutoa takwimu za miti iliyokuwa hadi sasa kati ya hiyo miti milioni saba ingawa alieleza kuwa miti mingi iliyopandwa imekuwa licha ya uwepo wa changamoto ya utunzaji miti hiyo ikiwepo la miti kuliwa na mifugo.
Kanali Mtambi amesema kwa mwaka huu mkoa huo unatarajia kupanda miti milioni 13 huku akisema lengo hilo lazima lifikiwe kwani hakuna kikwazo chochote kwa maelezo kuwa katika mkoa huo zipo taasisi 25 zinazojishughulisha na upandaji wa miche na kuigawa katika jamii bila malipo.
"Kupanda miti ni jambo jingine na kuhakikisha hiyo miti inakuwa ni jambo jingine hivyo kwasasa tunakwenda na vyote kwa pamoja yaani kupanda na kuisimamia ili ikue,uwezo huo tunao na tayari nimeelekeza kwa watendaji kuanzia ngazi ya chini kujipanga na jambo hilo," amesema
Amesema suala la athari za mabadiliko ya tabia nchini linapaswa kufanyiwa kazi kwa uhakika zaidi ili kunusuru mkoa na nchi kwa ujumla na majanga yatokanayo na mabadiliko hayo ya tabia nchi.
Amesema kampeni ya upandaji miti ndani ya mkoa kwasasa ni endelevu na kuanzia mwaka huu upandaji huo utafanyika kila mwezi ili kuhakikisha lengo hilo la kupanda miti milionin13 linafikiwa tofauti na kilindi cha nyuma ambapo kampeni hiyo ilikuwa ikifanyika mwezi Januari pekee .
"Kama nilivyosema tunataka miti yote inayopandwa inakua na ikitokea imeharibika basi iwe chini ya asilimia 5 tu tena kutokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wetu," amesema Kanali Mtambi.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka akipanda mti katika Shule ya Msingi Buhare Kati wilaya Musoma ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa mkoa wa Mara kupanda miti milioni 13 mwaka 2026. Picha na Beldina Nyakeke
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema wilaya yake ina lengo la kupanda miti milioni tatu mwaka huu na kwamba ili kuhakikisha miti hiyo inakuwa wanatarajia kuanza utekelezaji wa sheria ndogo ndogo za uhifadhi wa mazingira katika wilaya hiyo.
"Kuna wale wenye mifugo ambao wamekuwa na tabia ya kuacha mifugo yao kuharibu miti inayopandwa,tayari tunazo sheria ndogo ndogo za kushughulikia masuala hayo na lazima utekelezaji wake uanze ili kunusuru miti hii," amesema
Chikoka amesema wilaya hiyo kupitia kauli mbiu ya Musoma ya kijani kabla ya kuanza kutekeleza sheria hizo ndogo watendaji wataanza kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira ili kila mwananchi aweze kushiriki kikamilifu.
Ofisa wa Wakala wa Misitu Wilaya ya Musoma, Boniface Kaberege amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita wameweza kupanda miti zaidi ya 3,000 katika wilaya ya Musoma.
Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili kugawiwa miche ya miti inayotolewa na wakala huyo bila malipo yoyote.
"Tunaendelea na kampeni yetu ya upandaji miti na kwa leo kwenye hii Shule ya Msingi Buhare Kati tunatarajia kupanda miti 1,000 ya vivuli,matunda na mbao,nitoe wito kwa taasisi hizi ambazo tunazipa miti kusimamia ukuaji wake na hili likifanyika kwa ufasaha tutafanikisha kauli mbiu ya Musoma ya kijani,"amesema
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Buhare Kati, Arafa Mahimbo amesema chagamoto kubwa wanayokutana nayo katika utunzaji wa miti shuleni hapo ni uvamizi wa mifugo kwenye miti inayopandwa.
"Shule yetu ina miaka miwili sasa tumejitahidi sana kupanda miti lakini ile ya matunda imeshindwa kukua kwani imeliwa na mifugo ambayo huingizwa na wafugaji nyakati ambazo wanafunzi na walimu hawapo katika mazingira ya shule," amesema