Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi wafunga barabara baada ya mwanafunzi kugongwa

Muktasari:

  • Wananchi wameweka mawe katika barabara kuu ya Iringa – Mbeya ili kushinikiza mamlaka za serikali kuweka matuta katika eneo hilo kwa sababu kumbukumbu zinaonyesha kwamba eneo hilo limekuwa na matukio mengi ya ajali.

Iringa. Wakazi wa mtaa wa Kibwabwa, kata ya Kitwiru iliyopo katika halmsahauri ya manispaa ya Iringa wamefunga barabara kuu ya Iringa – Mbeya ili kushinikiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) kuweka matuta katika eneo hilo baada ya mwanafunzi mmoja kugongwa na gari.

Mwanafunzi huyo aliyetambulika kwa jina moja la Baraka, amegongwa na gari aina ya Hiace na kufariki njiani wakati akipelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.

Wakizungumza katika eneo la ajali leo February 18, 2022 wananchi hao wamesema mtoto huyo alikuwa amepandishwa kwenye Bajaji kwa ajili ya kupelekwa shule na dereva Bajaji alimpofikisha jirani na shule akamshusha na kumuacha avuke barabara.

Mashuhuda wanaeleza kwamba wakati mtoto huyo akivuka barabara, upande wa pili lilitokea basi dogo aina ya Hiace likamgonga mtoto huyo na kisha kwenda kuigonga Bajaj.

Wananchi hao wameamua kufunga barabara hiyo kwa kuweka mawe wakieleza kwamba eneo hilo limekuwa na mfululizo wa ajali licha ya kuiomba serikali kuweka matuta katika eneo hilo la kuvukia, hata hivyo haijachukua hatua yoyote.

Mmoja wa mashuhuda, Ashura Kalinga amesema hilo ni tukio la tatu kutokea katika eneo hilo na walimuomba diwani wa kata hiyo, Dk Hamza Mwamhehe kufanya utaratibu wa kuweka matuta lakini mpaka sasa bado hajachukua hatua.

“Tunamuomba diwani wetu atusaidie kutusemea tupate matuta katika eneo hili kwa sababu hili sio tukio la kwanza kutokea hapa, ikumbukwe eneo hili wanafunzi wanavuka kwa ajili ya kwenda shule, hivyo tunaiomba serikali na Tanroads kuchukua hatua kuokoa watoto wengine,” amesema.  

Festo Kaduma, mkazi wa kitwiru, ameiomba serikali wawawekee matuta makubwa ambayo yatakilazimisha kila chombo cha moto kupunguza mwendo na kuruhusu waenda kwa miguu kupita bila shida yoyote.

Akizungumza diwani wa kata ta Kitwiru, Dk Hamza Mwamhehe amesema tayari juhudi za kuyarudishia matuta katika barabara hiyo zinaendelea huku wakiiomba serikali kuweka matuta karibu karibu na kuweka kituo cha kuvukia watoto wa shule.

“Matuta yapo ila yamelika kutokana na uzito wa magari yanayopita, kwa hiyo kitakachofanyika ni kuyarudishia matuta na sasa yatawekwa matuta ya zege kwa kuwa matuta ya lami yanalika haraka na kutoweka.

Mwamhehe amewataka wazazi na walezi wa watoto kuwa waangalifu kwa watoto wao pindi waendapo shule na kuhakikisha wamevuka barabara salama ili kuondoa hofu ya watoto kuvuka barabara na kugongwa.

“Nawaomba wazazi na walezi wote wazingatie usalama wa watoto wao pindi waendapo shule na sio kuwaacha watoto wadogo chini ya miaka mitano kuvuka barabara wenyewe bila kuwahakikishia usalama wao,” amesema.