Wananchi wafurika madukani kutafuta vifaa vya kujikinga na maambukizi ya corona

Mkazi jijini Dar es Salaam akiwa eneo la Posta mpya jijini Dar es Salaam leo akiwa amevaa barakoa (maski) kwa ajili ya kujikinga na virus vya Corona. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Watu watufurika kwenye maduka ya madawa kusaka vifaa vya kujikinga na corona. Bei za vifaa hivyo zapanda maradufu

Dar es Salaam. Bidhaa za kusafisha mikono, gloves na barakoa (maski) za kufunika pua na mdomo zimeanza kuadimika huku bei zake zikipanda.
Hilo limeonekana baada ya kuthibitishwa kuwa Tanzania ina mgonjwa mmoja wa corona.


Katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam watu wameonekana wakiwa wamefunika pua na midomo yao kujikinga na ugonjwa huo.


Mwananchi ilitembelea mtaa wa Gerezani ambako kuna maduka makubwa ya dawa na kushuhudia watu wakifurika kwenye maduka hayo.


Hitaji kubwa la watu hao ni mask na sanitizer kwa ajili ya kusafisha mikono na kujikinga dhidi ya virusi vya Covid-19.


Katika maduka hayo yanayoamika kuwa na mzigo wa kutosha mengi yalikuwa hayana bidhaa hizo huku na pale zilipokuwepo bei yake ikipanda maradufu.
Sanitizer za mililita 60 zinauzwa kwa Sh12,000 huku kubwa za mililita 5,000 zikiuzwa kati ya Sh35,000.


Upande wa barakoa boksi moja lenye mask 20 linauzwa kati ya Sh80,000 hadi Sh130,000.
“Hapa mask ninazo bei yake ni Sh100,000 kwa boksi zinakaa 20 na sanitizer zipo za Sh35,000 na Sh40,000,” amesema mhudumu katika duka la dawa.
Bei hizo zimeonekana kuwaumiza vichwa watu waliofurika dukani hapo na wachache waliomudu walinunua huku wengine wakiondoka kwa simanzi.


Mkazi wa Kawe, Edgar Ngoda ni miongoni mwa waliofika kusaka bidhaa hizo lakini ameshindwa kumudu gharama.


“Namuomba Mungu atulinde maana ninachokiona kwa gharama hizi watu wengi tutakufa, mtu wa kipato cha kawaida atawezaje kumudu,” amesema Ngoda.