Wananchi walalamika viuno kuuma ubovu wa barabara Mufindi

Muktasari:


  • Wananchi wa Balali walalamia mkandarasi kushindwa kukamilisha ujenzi wa barabara Ihongole kwa wakati.

Mufindi. Wananchi wa Mtaa wa Balali, Kata ya Boma Halmashauri ya Mji Mafinga wamelakamikia Mkandarasi wa Kampuni ya Rahda Investment kushindwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa kipande cha barabara ya Balali kwa wakati hali ambayo imepelekea kuleta adha kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo.

Ubovu huo wa barabara umesababisha baadhi ya wananchi kushindwa kupanda Bajaj kutokana na kuumia viuno hivyo kuamua kutembea.
Barabara hiyo inatokea sokoni kwenda kituo cha Afya Ihongole kupitia Mtaa wa Balali ambapo imekuwa kero kubwa kwao wananchi wa maeneo hayo hali ambayo iliwalazimu kupaza sauti zao ili waweze kusaidiwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi leo Jumatano 25, 2023 Mkazi wa Ihongole na dereva Bajaji, Patrick Chang'a amesema kuwa barabara hiyo imekuwa kero kubwa kwao kutokana na mkandarasi kushindwa kukamilisha kwa wakati hali ambayo inasababisha msongamano mkubwa kwenye barabara hiyo.
"Hii barabara imekuwa kero kwetu hasa kipande hiki cha balali kutoka sokoni kwenda kituo cha afya Ihongole sisi madereva ambao tunatoa huduma ya usafiri bajaji zetu zinaharibika kwa sababu ya ubovu wa barabara hivyo tunaomba Serikali iingilie Kati kuhusu suala hili," amesema Chang'a.
Amesema kuwa barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kutokana wanasafirisha watu mbalimbali na wagonjwa pamoja na akina mama wajawazito kwa ajili ya kuwapeleka Kituo cha Afya Ihongole kupata matibabu.

" Huyu Mkandarasi ambaye amepewa hii barabara ametukosea sana...kwa sababu akina mama wajawazito wanateseka hata ukiendasha taratibu kwa namna barabara ilivyo hawezekani," amesema Kinyanga.
Mmoja wa wakazi wa Ihongole, Aloni Kinyaga amesema kuwa wanashindwa kupita vizuri kwa sababu mkandarasi amepanga nawe kwenye barabara hiyo kwa muda mrefu kwa kipindi cha miezi minne hadi sasa.
"Hii barabara mvua inaponyesha tunapata adha kubwa ya kubadilisha vikombe kutokana na kuharibika kwenye Bajaji zetu. Hii ni changamoto hata mzunguko wa biashara umedorora kwa sababu ya abiria hawezi kupanda wakati anaona anateseka hivyo wengi wanaamua kutembea kwa miguu," amesema Kinyaga.
Diwani wa Kata ya Boma, Julist Kisoma amesema kuwa barabara hiyo ilitakiwa kakamilika Januari 15 mwaka huu lakini hadi sasa bado haijakamilika.
Diwani hiyo amesema mikataba ya ujenzi wa barabara hiyo ulisainiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijiji (TARURA) Mkoa wa Iringa hivyo inakuwa vigumu kuwachukulia hatua.

Amesema baada ya wananchi kuona ujenzi huo umechelewa kukamilika walilazimika kuondoa mawe ambayo yalipangwa kwa ajili ya Ujenzi huo kuyaondoa ili waweze kupita kwa urahisi.

" Wananchi waliondoa mawe kwenye barabara hapa gharama zinaanza upya kwa sababu mawe walikuwa wameyapanga na ilibaki kazi ya kuweka kifusi tu ili wananchi waanze kupita kuendelea kufanya shughuli zao," amesema Kisoma.

Akijibu kero hiyo msimamizi wa barabara hiyo, Mhandisi wa Kampuni ya Rahda Investment, Francis Mnyambogwe amesema sababu ya kuchelewa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ni kutokana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha.
" Kwa sasa tumerudi tupo sehemu ya ujenzi ila kwa sasa tutaondoa mawe kwa ajili ya greda liweze kusafisha na tupange mawe tena upya na kifusi ili kuwapunguzia adha ya usumbufu wananchi kuhusu barabara hii," amesema Mnyambogwe.