Wananchi walia na daraja lililokatika miaka 10 iliyopita

Mwonekano wa daraja la mto Isenga linalounganisha vijiji vya Ilanga wilaya ya Ileje na Namwangwa wilaya ya Mbozi likiwa limebomoka.

Muktasari:

  • Daraja hilo lipo kwenye Mto Isenga ni kiunganishi kati ya vijiji vya Namwangwa Wilaya ya Mbozi na Ilanga Wilaya ya Ileje Mkoa wa Songwe ambazo wananchi hutegemeana kiuchumi.

Songwe. Wananchi wa Kata ya Hezya na Mlale Mkoani Songwe wameiomba Serikali kurejesha miundombinu ya daraja linalounganisha vijiji viwili vya kata hizo lililobomoka miaka 10 iliyopita.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti leo Jumatatu Aprili 15, 2024, wanasema wanateseka kusafirisha mazao yao kwenda sokoni kwa miaka 10 sasa.

Winifredi Simbeye Mkazi wa Kijiji cha Namwangwa amesema tangu daraja hilo  lisombwe na maji ya Mto Isenga mwaka 2013, kila msimu wa mvua ufikapo, wananchi wanaolima upande wa pili wanashindwa kuvuka kwenda kusimamia mashamba yao wakihofia kusombwa na maji.

"Mpaka sasa inasadikiwa zaidi ya  watu watano wamepoteza maisha kutokana na kutokuwepo kwa daraja hilo baada ya kusombwa na mafuriko walipokuwa wakivuka kwenye maeneo ambayo hayana kivuko rasmi,” amesema Simbeye.

Sara Mwampashi mkazi wa Kijiji cha Ilanga amesema mvua zinaponyesha, mto huo hufurika maji na kusababisha kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii kwa wananchi wa vijiji hivyo ambao hutegemeana.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilanga, Mfano Kayuni amesema daraja hilo ni kiungo muhimu kwa wananchi wa vijiji hivyo kwa kuwa shughuli nyingi za kiuchumi wanazifanya kwa kutegemeana hususani  za kilimo.

Akizungumzia kero hiyo, Diwani wa Mlale Wilayani Ileje, Yotamu Ndile amesema tayari Serikali imetoa fedha Sh2 bilioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hilo hivi karibuni, baada ya kutambua adha inayowakumba wananchi hao kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

“Nimewasiliana na Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini Wilaya ya Ileje (Tarura) Lughano Mwambingu na Mbunge wa Jimbo la Ileje na Naibu waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya  wamesema tayari  wametangaza tenda kupitia tangazo la mtandaoni ili apatikane mkandarasi atakayejenga daraja hilo,” amesema Ndile.

Akizungumzia suala hilo kwa njia ya simu na Mwananchi Digital,  Meneja wa Tarura Wilaya ya Ileje, Mhandisi  Mwambingu amesema fedha  hizo zimeshatengwa na Serikali na  wanatarajia kuanza ujenzi Juni mwaka huu.