Wananchi walia Polisi kuwatesa

Bahi. Wananchi na viongozi wa kijiji cha Chipanga A katika Wilaya ya Bahi wamelalamikia walichokiita mateso na maumivu wanayopata kutoka kwa Polisi Kata, Masunga Mnada.

 Ofisa huyo analalamikiwa kutumia muda mwingi kwenye mashamba yao akisuluhisha migogoro ya ardhi na kukata mipaka, huku akizikataa kamati za ardhi kuwa hawana uwezo wa kusuluhisha.

Anatuhumiwa pia kuwatoza wananchi fedha ili kumaliza kesi ofisini kwake na kutopeleka kesi mahakamani.

Hata hivyo Mnada, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu tuhuma hizo ikiwemo ya kuivunja Sungusungu kwenye Kata, alisema aulizwe Mkuu wake wa Polisi Wilaya atakuwa na majibu.

“Mimi si msemaji, lakini kwa taarifa zaidi nakupa namba ya OCD (Mkuu wa polisi wilaya) atakupa ufafanuzi wote unaotaka,” alisema Masunga.

 Mwananchi, lilipowasiliana na OCD Idd Ibrahim, alisema hajawahi kupelekewa malalamiko ya aina yoyote kuhusu Polisi huyo iwe kwa maandishi au kwa mdomo.

 Alisema kama yapo malalamiko kuhusu Ofisa huyo ni vema wanaolalamika wakajitokeza ili haki ifanyike na sheria ichukue mkondo wake.

 Mwananchi, pia liliwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno ambaye alisema anafuatilia suala hilo.

 Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni kijijini hapo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chipanga A, Samwel Mlewi alisema kwa sasa ofisi yake na Mtendaji hawana wanachokifanya kutokana na kumuogopa ofisa huyo, ambaye mara kadhaa hufika ofisini hapo na kuchukua kesi zote za usuluhishi.

 Mlewi anaeleza uamuzi wa Ofisa huyo wa Polisi wa kuwa msuluhishi wa migogoro umeshindwa kumaliza mzozo badala yake umeongeza zaidi.

Alisema kilio kikuu ni kwa wananchi wanaopelekwa kituoni wakiwa na tuhuma mbalimbali ambapo amejipa utaratibu wa kuwachapa kuanzia fimbo nane na kuendelea kisha mtu anatakiwa kulipa faini ili kesi zimalizwe.

 "Siyo wananchi tu, alimpiga Mwenyekiti wa Kitongoji hadi akawa hoi na akalipa Sh150,000. “Desemba 10 mwaka huu nilikwenda kuamua ugomvi wake na mama mmoja kuhusu mipaka ya ardhi akanirukia na kunikaba sana, kifupi hatuelewi pa kutokea," alisema Mlewi.

 Naye Mtendaji wa Kijiji hicho, Augustino Apolinary alisema kwa sasa anafanya kazi kwa mashaka kwani Polisi huyo akifika ofisini kwake huwa anapata hofu kubwa asijue anakwenda kufanya nini.

 Agustino alisema mambo mengi yanakwama kwa sababu watu wanamuogopa Masunga kwa hofu ya kubambikiwa kesi ili watishwe na kulipa Fedha.

 Mtendaji huyo alisema utendaji kazi wake umekuwa mgumu kutokana na Polisi huyo asiyetaka kushirikiana na viongozi wenzake ndani ya Kata.

 "Mimi nilichapwa viboko hadharani nilipokwenda kumdhamini mume wangu aliyekaa kituoni siku mbili kwa kosa la kumtukana mtu wakiwa kilabuni, nilikuta mume wangu anapigwa sana baada ya kukosa Sh300,000 nilipohoji somo likageuka," anasema Russia Nollo.

 Mama huyo anasema katika maisha yake hajawaji kupigwa na mikanda kama siku hiyo jambo alilosema linamfanya awakumbuke Polisi waliowahi kufanya kazi hapo na kuwa msaada.