Wananchi waliokosa maji kwa miaka 50 wakumbukwa

Muktasari:

  • Wananchi hao wanatumia maji ya kwenye madimbwi kutokana na kijiji hicho kutokuwa na maji safi na salama, umeme, na mawasiliano na hulazimika kwenda kijiji cha jirani  ili kufanya mawasiliano au kupanda kwenye miti kupata mtandao.

Mwanga. Wananchi zaidi ya 700 katika Kijiji cha Mwai, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro wataondokana na adha ya ukosefu wa maji safi na salama baada ya serikali kupelekea mitambo ya kuchimba kisima cha maji kitakacho gharimu zaidi Sh20 milioni.

 Kwa sasa wananchi hao wanatumia maji ya kwenye madimbwi kutokana na kijiji hicho kutokuwa na maji safi na salama, umeme, na mawasiliano na hulazimika kwenda kijiji cha jirani ili kufanya mawasiliano au kupanda kwenye miti kupata mtandao.

 Akizungumza leo Jumatatu Oktoba 9, 2023  Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Abdalla Mwaipaya, wakati wa kupokea mitambo   kwa ajili ya uchimbaji wa maji kijijini hapo amesema kijiji kinakabiliwa na adha ya ukosefu wa maji, umeme na mawasiliano  kwa zaidi ya miaka 50.

Mwaipaya amesema kijiji hicho kinakabikiwa na adha ya ukosefu wa maji tangu kuanzishwa kwake na kwamba kwa sasa Serikali imeanza kutatua changamoto hizo ili kuwezesha  wananchi kupata huduma bora.

“Serikali imeleta mitambo ya kuchimba mabomba ya maji ili kutimiza azma ya serikali ya kumtua mama ndoo kichwani, hivyo imeanza na maji na mengine kama  umeme ambao pia haupo katika kijiji hichi,” amesema Mwaipaya.

Amesema mitambo hiyo ambayo imepelekwa katika kijiji hicho ni miongoni mwa mitambo 25 iliyonunuliwa na serikali kwa ajili ya kushughulikia changamoto za maji vijijini.

Mmoja wa wanachi hao zena Ngowi, ameshukuru Serikali kuwakumbuka wananchi wa Kijiji cha Mwai katika kilio chao cha ukosefu wa maji kwa muda mrefu, ambapo amesema wanawake wanalazimika kuamka saa kumi afajiri kutafuta maji ambayo siyo salama kwa afya za binadamu.

“Kwa kweli hatuamini kama wanawake  wa  Mwai tumekumbukwa na Serikali kwa kuwa hatujawahi kupatiwa huduma muhimu kama wananchi wengine lakini leo tumeona serikali imetuletea maji tunaamini sasa hata umeme tutaletewa pamoja na huduma ya mawasilianao,” amesema Ngowi.

Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Wilaya ya Mwanga,  Cristine Kessey amesema  uchimbaji wa kisima hicho utakamilika baada ya siku nne.

Amesema tayari utafiti wa uchimbaji wa maji ardhini umefanyika na wananchi walitoa ushirikiano ambao umewezesha kuanza kuchimba kisima hcho ambacho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi zaidi ya 630.

 Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Joseph Thadayo amesema kijiji hicho kina shida kubwa tatu ambazo ni maji, umeme miundombinu chakavu ya shule ambayo tayari imeshakarabatiwa na kujengwa madarasa mapya.