Wananchi wanaidai wilaya ya Kilwa Sh5 bilioni

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai

Muktasari:

  • Wananchi hao wanadai fedha hizo kutokana na kuchukuliwa maeneo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa miradi ya maendeleo

Dar es Salaam. Halmashauri ya Manispaa ya Kilwa mkoani Lindi inadaiwa zaidi ya Sh5 bilioni na wananchi wa wilaya hiyo.

Fedha hizo zinatokana na kuchukuliwa maeneo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Hayo yalisemwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai wakati wa warsha ya kujadili uwazi wa mikataba mbalimbali ikiwamo ya gesi iliyoandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Oxfam.

Alisema halmashauri hiyo imechukua maeneo ya wananchi na kuzipimia viwanja taasisi mbalimbali, huku wananchi wakitembea na barua zao ili kupata msaada waweze kulipwa lakini hadi leo hawajafanikiwa.

Alisema wananchi wa wilaya hiyo wanaidai halmashauri hiyo tangu mwaka 2005.

"Hivi karibuni tulikaa kikao na mkurugenzi, madiwani na mwenyekiti wa halmashauri ya Kilwa ili kuangalia jinsi gani ya kufanya ili wananchi waweze kulipwa fedha zao kwa kuwa tangu mwaka 2005 maeneo yao yamechukuliwa, kupimwana kuuzwa  wakati watu hawajalipwa," alisema Ngubiagai.

Alisema kuna maeneo mengine yamechukuliwa na taasisi za Serikali, mashirika ya umma na watu binafsi.

Mkuu huyo wa wilaya alisema wananchi waliotoa eneo la Mpala kwa ajili ya chanzo cha maji waliondoka ambapo Serikali ilitoa Sh5 milioni lakini baadhi walilipwa na wengine kuachwa.

“Wananchi walitoa ardhi hekari 2,400 maeneo ya Sigino kwa Kikosi cha maji cha Jeshi la Wananchi (TPDF) kwa ajili ya kujenga kambi yao lakini hadi leo hii hawajalipwa na wanadai Sh3 bilioni,” alisema

Pia Chuo Kikuu cha Kislamu Morogoro (MUM) kimechukua eneo la ardhi la Mpala ndani ya mji mdogo wa Kilwa Masoko ambapo wananchi wanalalamika hawajalipwa.

Alisema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limechukua hekari 850 kwa ajili ya mradi mkubwa wa gesi ambao utagharimu kiasi cha Sh3 trilioni ambapo waliwalipa wananchi wa wilaya hiyo awamu tatu mwaka 1990, 1991 na 2016, lakini baadhi wanaodai fidia zao hawajalipwa.

Kwa upande wake, Meneja wa kampeni ya taasisi ya Oxfam, Jovita Mlay alisema  kuna changamoto ya usiri wa mikataba mbalimbali ya Serikali kutokuwa na uwazi  jambo ambalo linasababisha watu kutoelewa kitu gani kinafanyika.