Wananchi waomba kufikiwa na mradi wa uboreshaji ardhi

Muktasari:

  • Mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi ni mradi ulio chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na utekelezaji wake ulianza mwaka 2022 na unatarajia kukamilika mwaka 2026. Lengo la mradhi huo ni kuimarisha usalama wa milki za ardhi.

Chalinze. Wananchi katika halmashauri ya mji mdogo wa Chalinze wameomba kufikiwa na mradi wa uboreshaji na usalama wa umiliki ardhi ili kupunguza migogoro ya ardhi, ujenzi holela na pia kuondokana na imani za Kishirikina.

Kwa sasa mradi huo ambao umewafikia wananchi katika kata mbili za Pera na Mbwilingu kati ya kata 15 katika halmashauri hiyo, umeonyesha mafanikio kwa wananchi katika kutatua baadhi ya migogoro mikubwa ya mipaka, mirathi, barabara mashamba na kuboresha makazi.

Mradi huo wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi ni mradi ulio chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na utekelezaji wake ulianza mwaka 2022 na unatarajia kukamilika mwaka 2026.

Lengo la mradi mradi huo ni kuimarisha usalama wa milki za ardhi kwa kuongeza idadi ya Watanzania wenye nyaraka za kumiliki ardhi kwa kuzingatia jinsia, kuimarisha miundombinu ya msingi ya usimamizi wa ardhi, kujenga uwezo kwa watendaji na mamlaka za usimamizi wa ardhi pamoja na kutoa elimu ya masuala ya ardhi kwa wananchi.

Akizungumzia mradi huo leo, mkazi wa Chalinze, Anna Anatori ameiomba Serikali kuwafikia wakazi wengi ambao wanakabiliwa na migogoro ya ardhi huku akieleza kwamba yeye na familia yake wametumia zaidi ya miaka 10 kutafuta ufumbuzi, jambo ambalo lilisababisha waamini kwamba nguvu za kishirikina zinatumika wao kukosa haki.

“Kabla ya mradi tulikuwa na mgogoro mkubwa wa kifamilia baada ya baba yetu, marehemu kwa sasa, kupatiwa eneo kubwa na mzazi wake ambalo lilisababisha mgogoro na ndugu zake  na mzee alifariki kipindi hicho, hivyo tuliamini amerogwa lakini baada ya  mradi huu ulivyotufikia na kupata haki yetu, imetusaidia sana,” amesema.

Kwa upande wake, Clemence Joseph, mkazi wa Pera, ameshukuru kufikiwa kwa mradi huu ambapo elimu waliyopata kabla ya uhakiki na upimaji kuanza liliwasaidia katika kutatua migogoro ya mipaka na kuwafanya watoe maeneo ya mitaani ambayo yalikuwa hayana barabara, sasa yanafikika kwa urahisi zaidi.

“Mwanzo ilikuwa kupita eneo ambalo halina barabara mtaani kunazua mgogoro, sasa mambo yamebadilika baada ya uwekaji mawe, hata likitokea janga la moto ni rahisi gari kuingia na kutoa huduma kwa haraka.

“Kwa sasa vitongoji vingi bado havijafikiwa na mradi huu tuomba tufikiriwe ili maeneo ambayo yana migogoro yakiwemo maeneo ya mashambani yaweze kusaidika na muda uliotolewa ni mdogo,” amesema.

Nae kaimu katibu wa bodaboda kata ya Bwilingu, Juma Rashid ameshukuru pia mradi huo kwa kuwafikia vijana kwa kupata elimu ambayo itawasaidia kujua umuhimu wa uboreshaji salama wa umiliki ardhi ambao utaenda kuwainua kiuchumi.

“Tutakapopata hati zetu zitatusaidia kupata mikopo kwenye mabenki ambayo tutaifanyia biashara au kujenga nyumba, hivyo tunaomba mradi huu upongezwe sababu Chalinze ni kubwa na ndio mji unaokua,” amesema.

Kwa upende wake, Kaimu Mkuu Idara ya Ardhi, Deo Msilu amesema kwa sasa mradi umeweza kuhakiki vipande 11,000 ambapo wameweza kupima viwanja 750 na wameweza kuvuka lengo la kupima vipande 10,000 kwa miezi sita na lengo kuu ni kufikia vipande 50,000.

“Mahitaji ni makubwa kwa halmashuri ya Chalinze kwa sababu ilikuwa haijapangwa, hivyo tunahitaji viwanja zaidi ya 100,000 ili tuweze kuendana na malengo ya Serikali ya kimkakati, hivyo kwa sasa tumeanza kata hizi mbili na vitongoji vyake na tumefikia kata tatu tu ila lengo liko palepale kufikia kata zote zikiwemo kata ya Lugoba, Ubena, Vigwaza, Miono na Kiwangwa,” amesema.