Wananchi waomba vifaa vya kunawa mikono sokoni, stendi kuu Bukoba

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Wafanyabiashara na wananchi wanaofika kupata huduma katika Soko Kuu na Stendi Kuu Manispaa ya Bukoba wameomba Serikali kurejesha miundombonu ya maji na vifaa vya kunawa mikono katika maeneo hayo kama ilivyokuwa wakati wa janga la Uviko-19 kwa lengo la kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Marburg

Bukoba. Wafanyabiashara na wananchi wanaofika kupata huduma katika Soko Kuu na Stendi Kuu Manispaa ya Bukoba wameomba Serikali kurejesha miundombonu ya maji na vifaa vya kunawa mikono katika maeneo hayo kama ilivyokuwa wakati wa janga la Uviko-19 kwa lengo la kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Marburg.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti leo Ijumaa, Machi 24, 2023 wananchi hao wameomba miundombinu na vifaa hivyo kurejeshwa ili kuwawezesha kunawa mikono kama inavyoelekezwa kwenye kanuni za afya ikiwa ni moja ya mbinu ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo ambao tayari umeuwa watu watano mkoani Kagera.

“Moja ya kanuni za kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Marburg ni kunawa mikono kwa maji na sabuni. Ni muhimu kurejesha miundombinu na vifaa vya kunawa mikono vilivyokuwepo Soko Kuu na Stendi Kuu wakati wa janga la Uviko-19,”amesema Erenestina Kachonka, mmoja wa wajasiliamali Soko Kuu mjini Bukoba

Pamoja na kurejesha miundombinu na vifaa vya kunawa mikono, Mjasiriamali huyo pia ameshauri kila mtu kuchukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya maambukizi ikiwemo kutumia vitakasa mikono.

“Kila mwenye uwezo wa kununua vitakasa mikono afanye hivyo kujilinda,” ameshauri Kachonka

Hamdun Abdul, mkazi wa Manispaa ya Bukoba ameshauri vifaa vya kunawa mikono viwekwe kwenye kila lango la kuingia na kutoka katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwemo masoko, vituo vya mabasi, nyumba za ibada na hata kwenye misiba.

Uchunguzi wa Mwananchi katika maeneo ya Stendi na Soko Kuu mjini Bukoba umebaini kuwa miundombinu ya maji na vifaa vya kunawia mikono vilivyowekwa kwenye milango ya kuingia na kutoka kwenye maeneo hayo vilivyowekwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Bukoba (Buwasa) wakati wa janga la Uviko-19 havifanyi kazi.

Meneja wa Buwasa, John Shirat hajapatikana kuzungumzia mikakati ya kurejesha miundombonu hiyo baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kujibiwa.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Bukoba Alhamisi Machi 23, 2023, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Tumaini Nagu alitangaza mikakati ya Serikali ya kuweka miundombinu ya maji na vifaa vya kunawa mikono katika maeneo yote ya umma ikiwemo masoko, vituo vya mabasi, uwanja wa ndege na bandarini kama njia ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Marburg.

Ugonjwa wa Marburg tayari umesababisha vifo vya watu watano katika Kata ya Maruku na Kanyangereko Halmashauri ya Bukoba vijijini huku wengine watatu wakibainika kuambukizwa na wanaendelea kupatiwa matibabu.

Miongoni mwa dalili za ugonjwa huo ni kutapika au kutapika damu, homa kali, kuharisha au kuharisha damu, kuumwa kichwa na kutokwa damu sehemu mbalimbali za mwili.

Hadi kufikia Alhamisi Machi 23, 2023, jumla ya watu 193 waliochangamana na waliobainika kuwa na ugonjwa huo walikuwa wamewekwa karantini kama njia ya kuzuia maambukizi.