Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi wataja wanayotarajia kwa Rais akihitimisha mbio za Mwenge

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumza leo Oktoba Mosi 2024 na waandishi wa habari kuhusiana na ujio wa mwenge wa uhuru na kilele chake kitakachofanyika mkoani humo Oktoba 14, 2024. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

  • Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu kinatarajiwa kufanyika mkoani Mwanza Oktoba 14 katika Uwanja wa CCM Kirumba

Mwanza. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuhitimisha mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2024 mkoani Mwanza, baadhi ya wananchi wametaja wanayotamani ayazungumzie, kutolea maagizo, ufafanuzi na kuyatatua.

Kilele cha mbio hizo mwaka huu kinatarajiwa kufanyika mkoani Mwanza Oktoba 14 katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wakazi wa jiji wamesema shauku yao ni kusikia Rais Samia akitatua changamoto ya maji, akisisitiza uwajibikaji kwa viongozi na watumishi wa Serikali, ubovu wa miundombinu ya barabara, ugumu wa maisha, suala la ajira, kauli chafu kwa baadhi ya viongozi, mikopo na migogoro ya ardhi.

Mkazi wa Isamilo, Dua Nyauko akizungumzia uwajibikaji kwa watumishi na viongozi wa Serikali amedai kuwa, sasa hivi  utaratibu wa kuwaona umekuwa mgumu kiasi cha kushindwa kupeleka kero zao.

"Kwa mwananchi wa kawaida ukienda kwenye taasisi za Serikali kumuona bosi wa idara ni ngumu mpaka unajiuliza, je sisi hatustahili? Wakati wewe unaambiwa bosi ana vikao ila wengine wanaingia na kuongea naye na kuondoka," amesema.

Hata hivyo, Nyauko ametaja changamoto ya ugumu wa maisha kuwa ni moja ya maeneo ambayo wananchi wanashauku ya kusikia Rais akitoa kauli ya matumaini kwa Watanzania.

Mkazi wa Kata ya Kiseke, Mary Msisi amesema, "nitakuwepo na natamani kumuona Rais Samia akiwa kama mlezi wetu, atujali sisi wajane kwa kutupatia mikopo ili tuendeleze maisha yetu, pia aboreshe elimu ya shule ya msingi maana watoto wetu wanasoma lakini tunatoa gharama kubwa sana ya michango midogo midogo mfano watoto wa darasa la nne wana michango mingi sana," amesema Mary.

Mkazi wa Buhongwa, Stephano Francis amesema anatamani kusikia kauli ya Rais Samia kuhusu changamoto ya uhaba wa maji na ubovu wa miundombinu katika baadhi ya maeneo jijini Mwanza kuwa inatatuliwa.

Ester Eliabu amemuomba Rais Samia kushughulikia changamoto ya ukosefu wa ajira nchini na migogoro ya ardhi kwa kuwa imekuwa tatizo kubwa.

Awali, akizungumza leo Oktoba mosi 2024 na waandishi wa habari,  Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema mwenge huo baada ya kupokewa Oktoba 6, utakimbizwa kilomita 627 katika halmashauri nane za mkoa huo na kilele chake kitahitimishwa na Rais Samia.

"Mwenge wa uhuru unaingia Mwanza Oktoba 6 mwaka huu, tunatarajia kuupokea katika Kijiji cha Nyamadoke Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema ukitokea Geita, kwa hiyo kuanzia siku hiyo mpaka Oktoba 13 utakimbizwa katika halmashauri zote nane za mkoa huu," amesema.