Wanaodaiwa kumiliki akaunti ya Sukununu 01 wakamatwa
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro
Muktasari:
- Watano wametiwa mbaroni kwa tuhuma za makosa ya kimtandao, wakiwamo waliokuwa wamiliki wa akaunti ya mtandao wa X iitwayo Sukununu 01, uliokuwa ukidaiwa kuwatukana viongozi.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limewatia mbaroni watu watano wanaotuhumiwa kwa makosa ya mtandao, wakiwamo waliokuwa wamiliki akaunti ya Mtandao wa X iitwayo Sukununu 01 inayodaiwa kuwatukana viongozi wa Serikali.
Waliokamatwa ni pamoja na Obadia Kwitega (35) mkazi wa Kigamboni na Issa Mwamba (28) mkazi wa Tabata Segerea, kwa tuhuma za kumiliki televisheni ya mtandaoni na Youtube iliyotambulika kwa jina la Jamii Digital, na akauti ya mtandao wa X iitwayo Sukununu 01.
Akizungumza leo Machi 14, 2024 jijini hapa, Kamanda wa Polisi kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema watuhumiwa hao wawili licha ya kumiliki mitandao hiyo, walikuwa wanasambaza taarifa za uongo na uchochezi kuhusu viongozi wakuu wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba.
“Kuna baadhi ya taarifa zao zilisomeka kupitia mitandao yao ‘Mkakati wa siri wa Januari Makamba kumng’oa Rais Samia 2025,” amesema.
Kamanda huyo pia amesema wanamshikilia Edwin Kasebele Marlin (24) mkazi wa Mapelele mkoani Mbeya anayetuhumiwa kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook na WhatsApp kuwa anafanya biashara ya vitenge na hivyo kujipatia pesa kwa udanganyifu kutoka kwa watu mbalimbali.
“Watuhumiwa hao wamekutwa wakiwa na simu saba na kadi za za simu 13 za kampuni mbalimbali ya simu ambazo wamekuwa wakitumia kama nyenzo ya kutekeleza uhalifu wao,” amesema.
Mbali na watuhumiwa hap, Kamanda Muliro amesema wamemkamata Honest Mgona (47) mkazi wa Mabwepande kwa kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kuwa ametumwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi), Mohamed Nchengerwa, kwa ajili ya kusambaza mitungi ya gesi kwa wananchi na baadaye kuwatapeli kwa kuwadai pesa za usafiri.
Katika hatua nyingine Jeshi hilo limemkamata Frank Mbetu (35) mkazi wa Ligula, Mtwara kwa tuhuma za kujifanya mtumishi wa Serikali ngazi ya Katibu Mkuu kiongozi na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kwa kuwarubuni watu kuwa angewapa kazi na kuwapandisha vyeo.
Kutokana na vitendo hivi vya kihalifu kwa njia ya mtandao, Polisi wamewatahadharisha wananchi kuwa makini na matumizi ya mitandao wakifuata sheria, kanuni na taratibu za matumizi sahihi ya mitandao.
“Tunawahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa kwenye kituo cha Polisi kilicho karibu ili hatua stahiki zichukuliwe haraka. Pia tunaomba wananchi kutotoa wasifu (CV), namba ya kitambulisho cha Taifa (NIDA) au vitambulisho, nywila au namba ya siri (PIN) kwa mtu yeyote bila kuwa na uhakika na kinachofanyika,” amesema.
Uchunguzi
Katika hatua nyingine, polisi wanachunguza tukio la kuuawa kwa mtoto wa miaka saba na aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Kibonde Maji B Mbagala na mwili wake kukutwa Machi 13, 2024 kwenye msitu ulio karibu na shule aliyokuwa anasoma.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda Muliro amesema mtoto huyo aliondoka nyumbani kwao na mtoto mwenzake Machi 12, 2024 saa 11:30 jioni.
“Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Polisi Kilwa Road kwa uchunguzi zaidi. Ufuatiliaji mkali unaendelea kumtafuta mtuhumiwa, watuhumiwa waliohusika ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao,” amesema.