Wanaodaiwa kuwaua mume, mke mbaroni

Muktasari:
Walikuwa wakituhumu kwa wivu wa mapenzi na ushirikina
Kigoma. Polisi wilayani Uvinza mkoani Kigoma, inawashikilia watu watano kwa tuhuma za mauaji ya mume na mke kwa kuwacharanga mapanga kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi na imani za ushirikina.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Fednand Mtui aliwataja wanandoa hao waliouawa kuwa ni Nyanda Masele na mke wake, Kwilabya Masasila.
Mtuo alisema miongoni mwa watuhumiwa wanaowashikilia, wamo ndugu wa jirani wa Masele.
Tukio hilo lililoibua sintofahamu miongoni mwa wakazi wa Kijiji cha Mpeta wilayani humo lilitokea juzi alfajiri.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji cha Mpeta, Ndawanya Rafaely alidai kuwa wauaji hao walivamia nyumbani kwa Masele na kumuua kwa kumcharanga mapanga yeye na mkewe kisha kutokomea kusikojulikana.
Rafaely alisema uchunguzi wa awali uliofanywa na uongozi wa kijiji kwa kushirikiana na vyombo vya dola, ulibaini kuwa wake watatu wa Masele walikuwa na mvutano wa muda mrefu, huku wakimtuhumu mwenzao Masasila kuwa anapendwa na mume wao kuliko wao.
“Mmoja wa wake hao (jina linahifadhiwa), alikuwa akimtuhumu mke mwenzake huyo aliyeuawa kuwa ni mshirikina ndiyo maana anapendwa zaidi yao,” alidai Ndawanya.
Mmoja wa majirani wa familia hiyo, Majaliwa Magalinja alidai kusikia sauti za watu walipokuwa wanapiga kelele za kuomba msaada zikitokea nyumbani kwa Masele, usiku.
“Tuliamka na kwenda nyumbani kwa jirani yetu kujua wamekumbwa na nini.”
“Tukakuta mlango uko wazi, tuliingia ndani na kukuta mwili wa Masele sebuleni huku umetapaa damu na mkewe chumbani naye alikuwa ameuawa huku damu zikiwa zimetapakaa kitandani na sakafuni na wauaji walikuwa wametokomea kusikojulikana,” alidai jirani huyo.