Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanaodhaniwa wamekufa China wako gerezani

Balozi wa Tanzania nchini China, Suleiman Haji Suleiman akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Dawa za kulevya zimewafanya Watanzania wengi kufungwa nchini China. Wengine familia zao zimeamini wamefariki kwa sababu hawajapata taarifa zao kwa muda mrefu, lakini tunapofuatilia tunawakuta bado wako hai na wanatumikia vifungo vyao



Dar es Salaam. Wakati baadhi ya familia nchini zikiendelea kuomboleza, zikiamini kuwa ndugu zao waliokwenda China walifariki dunia baada ya kupoteza mawasiliano nao, imebainika kuwa baadhi yao bado wako hai wakitumikia vifungo virefu gerezani kutokana na makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.

Taarifa hiyo imetolewa na Balozi wa Tanzania nchini China, Dk Suleiman Haji Suleiman akisema biashara na matumizi ya dawa za kulevya vinaendelea kuwaangamiza Watanzania wengi wanaokwenda nchini humo kutafuta fursa za biashara.

Akizungumza leo Jumanne, Julai 14, 2026 na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) jijini Dar es Salaam, Dk Suleiman amesema ubalozi umekuwa ukifuatilia kesi nyingi za Watanzania waliokamatwa kwa makosa ya dawa za kulevya, huku baadhi ya familia zao zikipoteza matumaini kutokana na kukosekana kwa mawasiliano kwa muda mrefu.

Amesema hali hiyo imewafanya baadhi ya ndugu kuamini wapendwa wao walifariki dunia, ilhali bado wanaishi na wanatumikia vifungo katika magereza ya China.

"Dawa za kulevya zimewafanya Watanzania wengi kufungwa China. Wengine familia zao zimeamini wamefariki kwa sababu hawajapata taarifa zao kwa muda mrefu, lakini tunapofuatilia tunawakuta bado wako hai na wanatumikia vifungo vyao," amesema Dk Suleiman.

Balozi huyo amesimulia kisa cha mama mmoja aliyefika kwenye banda la Ubalozi wa Tanzania katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), akieleza kuwa aliamini mwanaye aliyekuwa China alifariki dunia.

Hata hivyo, amesema baada ya ubalozi kuanza kufuatilia taarifa hizo, ilibainika kijana huyo alikuwa hai na anaendelea kutumikia kifungo chake.

Balozi wa Tanzania nchini China, Suleiman Haji Suleiman akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga

"Alidhaniwa amefariki, lakini tulibaini yupo hai. Anatarajiwa kumaliza kifungo chake mwaka 2031," amesema.

Katika tukio jingine, Dk Suleiman amesema ubalozi ulifuatilia taarifa za mwanamke aliyekamatwa nchini China mwaka 2015 kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na baadaye kuhukumiwa mwaka 2019.

Amesema mwanamke huyo ambaye kabla ya kukamatwa alikuwa akifanya biashara ya vitenge kati ya Tanzania na China, anatarajiwa kumaliza kifungo chake mwaka 2045. Kwa muda mrefu familia yake ilikuwa imepoteza matumaini baada ya kushindwa kupata mawasiliano naye.

"Nawapa picha ndugu zangu kuwa suala la dawa za kulevya si la kuchezea. Watu wanaweza kuingia kwa urahisi, lakini madhara yake ni makubwa sana," amesema.


Mtego wa biashara

Dk Suleiman amesema baadhi ya Watanzania, hasa wanawake huingia katika biashara hiyo baada ya kuanza safari za kawaida za kibiashara kwenda China.

Amesema wengi huanza kwa kusafirisha bidhaa halali kama vitambaa, lakini baadaye hushawishiwa kubeba dawa za kulevya kwa ahadi ya kulipwa fedha nyingi.

"Anabeba vitambaa mara ya kwanza na ya pili, baadaye anashawishiwa kubeba 'unga.' Lakini China wana mifumo madhubuti ya ukaguzi. Ukijaribu kupitisha dawa hizo utakamatwa," amesema.

Amesisitiza kuwa, sheria za China kuhusu dawa za kulevya ni kali na hazitoi nafasi kwa mtu anayebainika kujihusisha na biashara hiyo.

Kutokana na hali hiyo, amewataka Watanzania wanaokwenda China kuwa waangalifu na kuepuka kubeba mizigo ya watu wasiowafahamu kwa ahadi ya kupata fedha.

"Sisi ubalozi tunaendelea kutoa elimu, lakini niwasihi vijana wajilinde. Wapo ndugu zetu wengi wanaoteseka magerezani kwa sababu ya dawa za kulevya. China hawana mchezo katika suala hili," amesema.

Ripoti ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini ya mwaka 2025, iliyotolewa Mei 2026, inaonyesha Watanzania 28 walikamatwa katika nchi mbalimbali duniani mwaka 2025 kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Zambia iliongoza kwa kuwakamata Watanzania wengi zaidi, ikiwa na watuhumiwa 20.

 Botswana na Msumbiji zilifuatia kwa watuhumiwa wawili kila moja, huku Mauritius, Japan, Ufaransa na Shelisheli kila moja ikiripoti kumkamata Mtanzania mmoja.

Akizungumza na Mwananchi, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amesema Watanzania wanaokamatwa nje ya nchi huhukumiwa kwa mujibu wa sheria za mataifa husika.

"Hawa watahukumiwa kulingana na sheria za nchi walizokamatwa. Kila nchi ina adhabu zake kwa makosa ya dawa za kulevya. Inawezekana huko walikokamatwa adhabu ikawa tofauti na Tanzania, ambako kwa sheria yetu ukikamatwa na dawa za kulevya unaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha," amesema.

Kuhusu hali ya China, Lyimo amesema mamlaka zinaendelea kushuhudia Watanzania wakikamatwa nchini humo, huku wengi wakidai kwenda kufanya biashara nyingine, lakini baadaye kutumika kama wasafirishaji wa dawa za kulevya.

Amesema wanawake ndio wanaoathirika zaidi, huku uchunguzi ukionyesha wengi wao husafirisha dawa hizo kwa kuzimeza au kuzificha katika sehemu mbalimbali za miili yao.

"Ufuatiliaji wetu unaonyesha wengi wanatumika kusafirisha dawa hizi, iwe kwa kumeza au kuzificha kwenye miili yao. Hii ni hatari kubwa kwa maisha yao. Wanaowatumia ndio wanaonufaika, lakini wao hupoteza uhuru, heshima na malengo yao ya maisha. Tumewahoji baadhi yao, unakuta mtu aliahidiwa Sh5 milioni na kulipiwa gharama za safari ili kusafirisha mzigo kwenda China. Fedha hiyo haiwezi kuwa na thamani kuliko utu na maisha ya mtu," amesema Lyimo.