Wanaoidai hoteli ya Impala, Naura Spring kulipwa hivi

Wanaoidai hoteli ya Impala, Naura Spring kulipwa hivi

Muktasari:

  • Mahakama kuu kanda ya Arusha imetoa hukumu ya kuuzwa viwanja vinne  vinavyomilikiwa na kampuni ya  Impala ili kuwalipa  wafanyakazi 238 wa hoteli ya Impala na Naura Spring zote za jijini Arusha wanaodai mishahara  zaidi ya Sh500 milioni.

Arusha. Mahakama kuu kanda ya Arusha imetoa hukumu ya kuuzwa viwanja vinne  vinavyomilikiwa na kampuni ya  Impala ili kuwalipa  wafanyakazi 238 wa hoteli ya Impala na Naura Spring zote za jijini Arusha wanaodai mishahara  zaidi ya Sh500 milioni.

Maamuzi hayo yametolewa jana Jumatatu Februari 8, 2021 na Jaji Mohamed Gwae ambaye pia  imeridhia maombi ya benki ya biashara ya NBC inayoidai hoteli ya Impala Sh1.5 bilioni kwamba fedha zitakazobaki baada ya mali za mdaiwa kuuzwa na kuwalipa wafanyakazi, benki hiyo nayo ilipwe.

Jaji Gwae alieleza kutoa hukumu hiyo baada ya kujiridhisha kwamba maombi yaliyoletwa na wamiliki wa hoteli hizo ya kupinga uamuzi wa msajili wa mahakama kuu Kanda ya Arusha, masjala ndogo ya kazi hayana mashiko.

Jaji Gwae aliamuru viwanja namba 20,21,22 na 23 vilivyopo block B Uzunguni  jijini Arusha kuuzwa na kufidia mishahara ya wafanyakazi hao ambao 68 wa hoteli ya Naura  wanaodai zaidi ya Sh107milioni na 167 wa hoteli ya Impala wanaodai Sh397 milioni.

Mwenyekiti wafanyakazi hao, Jacob  Joel amesema anashukuru uamuzi wa mahakama pamoja na Serikali kuwa na nao bega kwa bega hadi  kesi kufikia  hapo.

Amesema wana imani dalali wa mahakama,  Boniface Buberwa atafanya kazi  kwa uzalendo ili kumaliza mchakato wa kuuzwa kwa viwanja hivyo.

Impala, Naura Spring na Ngurdoto Mountain Lodge zilikuwa zinamilikiwa na Melau Mrema aliyefariki dunia  mwaka 2017.