Wanaotumia simu janja hii inakuhusu
Dar es Salaam. Kama unatumia simu janja hii ni ya kwako isikupite, Benki ya Exim Tanzania imezindua kampeni maalum inayolenga kuwashawishi wateja wake wanaomiliki simu za mkononi kufanya miamala zaidi kwa kutumia simu zao pamoja na kutumia mtandao badala ya malipo ya fedha taslimu pindi wanapohitaji kutumia huduma mbalimbali za kibenki.
Kampeni hiyo ya miezi mitatu itaambatana na zawadi mbalimbali ambazo zitatolewa kila wiki na mwezi kwa washindi.
Kampeni hiyo iliyopewa jina la 'Tap Tap Utoboe' inatoa fursa kwa zaidi ya washindi 200 miongoni mwa wateja wa benki hiyo wanaotumia simu zao au mtandao kufanya miamala, kuwa kwenye nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali ikiwemo fedha taslimu, pikipiki, bajaji pamoja na zawadi kubwa ya gari mpya aina ya Mazda CX-5.
Tap Tap Utoboe inalenga wateja wa sasa na wateja wapya. Kwa mteja ambaye hajawahi kutumia huduma za kibenki za simu za mkononi na mtandaoni, hii ni fursa yake kujiunga.
Aidaha, kwa wateja wapya, waalikwa kujiunga na familia ya Exim Benki na kufurahia huduma zao bora za kibenki za kidigitali. Ili kushiriki, mteja anatakiwa kufanya miamala yake yote ya kibenki kupitia simu yake au mtandao, ikiwamo kulipia ankara za maji, umeme au visimbusi vya television, malipo ya manunuzi, kutuma pesa, kulipia kodi, kutoa fedha kwa Exim Wakala, kulipia bima ya vyombo vya moto, na huduma nyenginezo.
Ili kushinda zawadi, mteja anahimizwa kufanya miamala ya mara kwa mara kupitia huduma za kibenki za simu za mkononi na mtandaoni.
Pia, washindi kumi wa kila wiki watapata Sh50,000 kila mmoja, na washindi kumi wa kila mwezi watapata Sh100,000 kila mmoja. Mshindi wa tatu atapata pikipiki, mshindi wa pili atapata bajaji, na mshindi wa kwanza na jumla ataondoka na gari mpya kabisa aina ya Mazda CX-5.
Kwa mujibu wa Exim wakati wa kampeni hiyo kila muamala wenye thamani ya Sh50,000 na zaidi ukiwa umefanyika kwa zaidi ya mara moja kupitia simu ya mkononi au mtandao, muhusika atastahili kushiriki bahati nasibu ya kumpatia mshindi.
“Kila wiki, kutakuwa na droo na wateja 10 watakaobahatika watapata nafasi ya kujishindia zawadi ya fedha taslimu Sh50,000,’’ ametaja, huku akiongeza: “Aidha, kila mwezi kutakuwa na droo ambapo wateja 10 watapata nafasi ya kujishindia fedha taslimu Sh100,000 huku sifa ya chini katika droo hii ya mwezi ikiwa ni mhusika kufanya miamala yenye thamani ya Sh200,000 na zaidi katika huduma moja au zaidi.''
Huduma za kibenki za simu na mtandaoni za Exim zimeundwa kurahisisha maisha ya mteja kwa kuhakikisha upatikanaji, urahisi, na usalama wa miamala yake. "Tunataka wateja wetu wafurahie urahisi na manufaa ya huduma za kidigitali huku wakiwa salama na kufurahia ufanisi wa miamala yao," amesema Lyimo.
Mkuu wa Njia Mbadala na Mabadiliko ya Kidijitali wa Benki ya Exim, Silas Matoi amesema, "Ubunifu wa kidijitali ni msingi wa mkakati wetu. Kampeni ya Tap Tap Utoboe imeundwa kuhusisha watumiaji wa teknolojia na wale wasioijua sana, kuhakikisha kila mmoja anafaidika na huduma zetu."
Naye, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Stanley Kafu alisema dhamira ya msingi ya benki hiyo ni kuandaa jamii yenye utamaduni wa kutotembea na pesa taslimu na badala yake wafanye miamala kwa njia za kielectroniki hatua ambayo pia imekuwa ikipigiwa chapuo na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidunia katika kufanya miamala ya kifedha.
“Benki yetu kihistoria imekuwa mstari wa mbele kuleta mageuzi ya kihuduma hapa nchini. Katika kufanikisha mageuzi hayo tumekuwa tukitumia namna mbambali ikiwemo kutoa zawadi kwa wateja wetu ili tu tuweze kwenda nao sambamba katika mageuzi haya.
Tunaamini kupitia kampeni hii tunakwenda kuleta mabadiliko yenye tija na faida kubwa kwenye mfumo mzima wa sekta ya fedha hapa nchini na iatawapa wateja wetu fursa ya kufurahia huduma za kibenki zenye urahisi wa matumizi, upatikanaji wa haraka, na uaminifu.
Hii ni sehemu ya kujitolea kwetu katika kuboresha huduma kwa wateja wetu na kuwahamasisha kutumia huduma zetu za kidijitali’’ alisema.