Wanaume Kitunda wadai kupigwa na wake zao

Wanaume Kitunda wadai kupigwa na wake zao

Muktasari:

  • Vitendo vya wanaume kunyanyaswa hasa wastaafu vimedaiwa kushamiri katika kata ya Kitunda mkoani Dar es Salaam na baadhi yao huishia kutoa malalamiko hayo katika vijiwe vya kahawa.

Dar es Salaam. Vitendo vya wanaume kunyanyaswa hasa wastaafu vimedaiwa kushamiri katika kata ya Kitunda mkoani Dar es Salaam na baadhi yao huishia kutoa malalamiko hayo katika vijiwe vya kahawa.

Wapo wanaopigwa na wake zao na wengine kusimangwa pamoja na kukatazwa kujumuika na wazee wenzao.

Akizungumza na Mwananchi Digital  jana Aprili 15, 2021 mraghabishi wa masuala ya ukatili wa kijinsia,  Ramadhani Mbegu Mkali amesema vitendo hivyo vilizoeleka kufanyika zaidi kwa wanawake na watoto, lakini sasa mambo yanabadilika.

Mzee Mkali mkazi wa Kitunda, amesema kwa miaka 10 amekuwa akishirikiana na taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali namna ya kutetea watu wanaonyanyaswa kijinsia lakini tathmini kuhusu wanaume wanaonyanyaswa kesi ndiyo zinaanza kuingia hivi sasa ambapo wanajitahidi kuzifanyia kazi.

Amesema ukatili huo upo lakini kinachoufanya usisikike, ni wanaume kutofika vituoni kuripoti huku wengine wakiona aibu hata kusimulia marafiki.

“Wanaume tumejijengea mila na desturi zisizokuwa nzuri, anaweza kuja kwangu kuripoti lakini kama akienda polisi akishaeleza wanaanza kuitana,  ona huyu mwanaume mkewe amempiga amekuja kuripoti,  kila mtu anakushangaa unaonekana kama vile ni kitu cha ajabu na hili linawakwamisha wengi wanarudi nyuma,” amesema.

Mkali amelitaja kundi linalokutana na ukatili zaidi kuwa ni wazee waliokuwa na fedha lakini baada ya kustaafu wamekuwa fedha hawana tena na kukaa kwao majumbani bila shughuli ndio chanzo, kuongeza kuwa wapo ambao hawana umri mkubwa lakini wanakumbana na hali hiyo.

“Kesi hizi tunazifuatilia hazijaletwa moja kwa moja ni wachache wanakuja, nyingi zinazungumzwa na sisi tunazipata sana kwa wazee wenzangu kwenye kahawa au misikitini utasikia aah bwana nyumba fulani na fulani inatawaliwa na mkewe anafanyiwa hivi na vile,” amesema.

Ofisa Mtendaji kata ya Kitunda, Beatrice Shio amesema suala hilo lipo limekuwa likisikika chini kwa chini lakini wanaume wamekuwa wazito kujitokeza hadharani.

“Nimewahi kupata kesi moja ambapo mwanaume alifika kwangu akashtaki mkewe anampiga,  tulivyomuuliza kwamba tunataka tumsaidie alikataa na kusema alikuwa anataka tu ushauri.”

“Tulimpeleka kwa ofisa ustawi wa jamii ili amshauri nini cha kufanya, tukamuita mkewe tukamshauri. Suala hili lipo miongoni mwa jamii lakini linafichwa fichwa,” amesema Shio.

Ofisa programu kutoka Shirika la Utu wa Mtoto (CDF),  Euphomia Edward amesema mbali na ukatili huo, taasisi yao imekuwa ikishirikiana na ubalozi wa Uholanzi nchini, wakijikita kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kupitia mradi ambao ulianza mwaka 2017.

Euphomia amesema katika maeneo wanayofanyia kazi kata ya Kitunda ni kati ya maeneo yanayoongoza katika ukatili.

“Tulipokutana na watendaji wamekiri kulikuwa na hiyo changamoto unyanyasaji wa wanawake na watoto, kesi za wanandoa, kugombania ardhi kuna masuala mengi ya ukatili ambayo yanaendelea katika kata hii,” amesema Euphomia.

Imeandikwa Herieth Makwetta na Salama Ringo, Mwananchi