Wanaume watatu wajinyonga Kilimanjaro, kisa msongo wa mawazo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa
Muktasari:
- Yumo mwenyekiti wa Kitongoji cha Kotela Mashariki, Lamecky Matowo (57), huku uchunguzi wa awali wa Polisi ukionyesha vifo hivyo vimechangiwa na msongo wa mawazo.
Moshi. Wakati mijadala kuhusu afya ya akili ikiendelea kushika kasi nchini, matukio ya wanaume watatu kujinyonga ndani ya siku mbili wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, yameibua wasiwasi kuhusu ukubwa wa tatizo hilo kwa wanaume na namna wengi wanavyokosa msaada hadi kufikia uamuzi wa kujiua.
Wataalamu wa afya ya akili wanasema wanaume wengi huishi na mizigo ya kifamilia, kiuchumi na kijamii wakiwa kimya kutokana na mila na mitazamo inayowataka waonekane imara wakati wote, hali inayowafanya baadhi yao kuchelewa kutafuta msaada wanapokumbwa na changamoto za kisaikolojia.
Hofu hiyo imekuja baada ya wanaume watatu kufariki dunia kwa kujinyonga, akiwamo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kotela Mashariki, Lamecky Matowo (57), huku uchunguzi wa awali wa Polisi ukionyesha kuwa wawili kati yao walikuwa wakikabiliwa na msongo wa mawazo na changamoto za afya ya akili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema matukio hayo yalitokea Julai 21 na 22, mwaka huu.
Amesema Matowo alikutwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya manila aliyokuwa ameifunga kwenye mti uliopo shambani kwake.
Mbali na Matowo, waliofariki ni Januari Hussein (30), dereva wa bodaboda na mkazi wa Kimaroroni pamoja na Frank Makundi (54), fundi ujenzi na mkazi wa Kijiji cha Komakundi, Kata ya Mamba Kaskazini.
"Uchunguzi wa awali umebaini kuwa Matowo alijiua kutokana na changamoto ya afya ya akili. Makundi naye alikumbwa na msongo wa mawazo baada ya kufiwa na mtoto wake miezi miwili iliyopita, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha kifo cha Januari Hussein," amesema Kamanda Maigwa.
Mdogo wa marehemu Matowo, Felix Matowo, amesema familia imepokea taarifa za kifo hicho kwa mshangao kwa kuwa ndugu yao hakuwa ameonyesha dalili zozote zinazoweza kuashiria alikuwa akipitia kipindi kigumu.
"Sijui nini kilichomsibu kaka yangu. Alikuwa hana tatizo lolote. Aliamka asubuhi akafanya shughuli zake za kawaida za kulisha mifugo, akanywa chai, halafu baadaye akaonekana kujitenga," amesema Felix.
Amesema mama yao alipojaribu kumtafuta hakumpata nyumbani na baada ya majirani kuanza kumtafuta walimkuta shambani akiwa amejinyonga.
Akizungumzia matukio hayo, mwanasaikolojia wa jamii, Hilda Mwakalonge, amesema matukio ya wanaume kujiua yanaonyesha ukubwa wa tatizo la afya ya akili ambalo mara nyingi halionekani hadi linapofikia hatua mbaya.
Amesema wanaume wengi wamelelewa katika mazingira yanayowafundisha kuficha hisia zao, kutolia na kutokiri wanapokuwa na maumivu ya kisaikolojia, jambo linalowafanya kubeba msongo wa mawazo kwa muda mrefu bila kupata msaada.
"Jamii imejenga dhana kwamba mwanaume anatakiwa awe mvumilivu na asionyeshe udhaifu. Matokeo yake, wengi wanapitia msongo wa mawazo, huzuni, upweke na hata sonona wakiwa kimya kwa hofu ya kuonekana dhaifu au kushindwa kutimiza wajibu wao," amesema Hilda.
Amesema changamoto za kiuchumi, migogoro ya kifamilia, madeni, kupoteza wapendwa, shinikizo la kuwahudumia wanafamilia na matatizo ya mahusiano ni miongoni mwa sababu zinazochangia wanaume wengi kuingia katika msongo wa mawazo.