Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanavijiji wawezeshwa kulinda misitu Tanga, Kilimanjaro

Ofisa Miradi wa Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF), Magreth Victor akizungumza katika hifadhi ya mazingira asilia ya Amani (Amani Nature Reserve). Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

  • Wanavijiji hao wanapewa fedha wa miradi rafiki ikiwemo ya upandaji miti, utengenezaji majiko sanifu, ufugaji wa samaki na nyuki ili kupunguza kasi ya uvunaji wa misitu kwa ajili ya kuni, kuchoma mkaa na kupasua mbao.

Muheza. Ili kulinda misitu wananchi wa vijiji 20 kutoka halmashauri tano zinazozunguka hifadhi ya misitu ya Amani mkoani Tanga, wananufaika na ajira ikiwemo za usafishaji wa mipaka na uboreshaji wa barabara na miundombinu mingine ya kuvutia utalii.

Vijiji hivyo vinatoka Wilaya za Muheza, Lushoto, Korogwe na Mkinga (Tanga) na Same mkoani Kilimanjaro.

Wanavijiji hao pia wanapewa fedha wa miradi rafiki ikiwemo ya upandaji miti, utengenezaji majiko sanifu, ufugaji wa samaki na nyuki ili kupunguza kasi ya uvunaji wa misitu kwa ajili ya kuni, kuchoma mkaa na kupasua mbao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Februari 21, 2024, Kaimu Mhifadhi wa hifadhi hiyo ya mazingira ya asilia ya Amani, Nikundiwe Majoya amesema miradi na ajira hizo kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo imesaidia kupunguza uharibifu wa misitu.

Amesema miradi hiyo inatekelezwa na mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF), imesaidia kuongeza mapato ya hifadhi hiyo kutoka Sh30 milioni kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 hadi kufikia Sh40 milioni mwaka 2023/2024 na idadi ya watalii katika kipindi hicho ikiongezeka kutoka 3,000 hadi kufikia watalii 4,000.

“Katika hifadhi hii tunahifadhi biaonwai zote ambazo zinapatikana katika msitu huu lakini kupitia ufadhili wa mfuko huo katika nyanja tofauti ikiwemo doria, ufanyaji usafi katika mipaka na  njia za watalii na miradi kwa jamii imesaidia kuilinda.”

“Tunaona maboresho ya viumbehai vinazidi kuboreka na hata vilivyokuwa vimetoweka awali sasa vimerejea katika hali yake ya kawaida hasa ndege na vinyonga ambao wanapatikana katika msitu huu, kutokana na kushirikisha jamii kwa kiasi kikubwa kuulinda,” ameongeza

Mmoja wa wanufaika wa ajira hizo, Mrisho Nzota kutoka Kijiji cha Mikwinini, Kata ya Shebomeza, ambaye anahusika na kusafisha mipaka na njia za watalii, amesema kutokana na elimu ya uhifadhi waliyopewa imewasaidia kutambua umuhimu wa utunzaji wa mazingira, huku ajira hizo zikiwapa kipato kinachowawezesha kuhudumia familia zao.

Amesema awali walikuwa wakiishi maisha magumu kutokana na kutokuwa na shughuli zinazowawezesha kujiingizia kipato ila kwa sasa imewasaidia hadi kuzuia viashiria vinavyoweza kuhatarisha usalama wa hifadhi na kushirikiana kulinda na kudhibiti eneo hilo.

Kwa upande wake Ofisa miradi wa Mfuko huo Kanda ya Kaskazini, Magreth Victor amesema kila mwaka wamekuwa wakitoa Sh49 milioni kwa hifadhi hiyo, kwa ajili ya kufanya shughuli za uhifadhi, utunzaji wa misitu pamoja na utalii ikolojia ikiwemo kusafisha mipaka, kufanya doria na kuboresha vivutio vya watalii ikiwemo malazi.

Naye mwongoza watalii katika hifadhi hiyo, Gabriel Ponera ametaja miongoni mwa vitu vichache vinavyovutia watalii ni pamoja na kinyonga mwenye pembe tatu anayepatikana katika milima hiyo pekee na baadhi ya ndege ambao hawaonekani kwa urahisi katika maeneo mengine.