Wanawake 474 wafanyiwa ukatili Babati

Wednesday October 06 2021
Ukatili pc

Muuguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Matilda Geay akizungumza na wanachama wa klabu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara (MNRPC) wanawake na wasichana wa Kata ya Riroda, kwenye mafunzo ya mradi wa haki ya afya ya uzazi uliofadhiliwa na taasisi ya Women Fund Tanzania Trust (WFT). Picha na Joseph Lyimo

By Joseph Lyimo

Babati. Imeelezwa kuwa wanawake 474 wamefanyiwa ukatili wa aina tofauti mwaka 2020 Mjini Babati Mkoani Manyara, ikiwemo ukatili wa kimwili uliotajwa kuwa na matukio 249, ukatili wa kingono matukio 48 na kijinsia matukio 117.

Ofisa ustawi wa jamii wa Halmashauri hiyo, Mathias Focus, ameyasema hayo leo Oktoba 6 wakati akizungumza na wanawake na wasichana wa kata ya Riroda waliopo kwenye mradi wa haki ya afya ya uzazi unaosimamiwa na klabu ya waandishi wa habari Mkoani Manyara (MNRPC) kwa ufadhili wa taasisi ya Women Fund Tanzania Trust (WFT).

Focus amesema katika matukio hayo, wanawake wamekuwa wakivutwa nywele kwa kukosea kupika na wengine kuambulia kipigo.

Soma hapa: Ukatili wa kijinsia washika kasi nchini

Amesema ukatili wa kihisia una athari za kisaikolojia, akitaja kauli za matusi zinazoleta fedheha kwa wanaofanyiwa akitoa mfano wa mtoto anapotukaniwa mzazi wake anapokuwa amekosea. 

"Wivu wa kupitiliza ni ukatili wa kihisia ambao unaathiri wanawake kisaikolojia kwa kuwa wapo ambao wanafuatiliwa kila wanachofanya," amesema Focus.

Advertisement

Amesema sababu za ukatili ni watu kuwa na jeuri ya uwezo wa kielimu au kifedha, kuwa na mamlaka, dini na migogoro ya kifamilia.

Ameyataja madhara ya ukatili kuwa ni majeraha, vifo, magonjwa ya zinaa na waganga kujitenga na jamii.

Ametumia fursa hiyo kuishukuru klabu ya waandishi wa habari kwa kuamua kutoa elimu kwa kundi hilo la wanawake kuanzia umri wa miaka 14 hadi miaka 70.

Soma hapa:

Kwa upande wake, muuguzi wa wilaya ya Babati, Matilda Geay amewashauri wakiwa wajawazito kuanza kliniki mara tu wanapopata ujauzito ili waweze kuhudhuria kliniki mara nane kabla ya kujifungua,

Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Mkoani Manyara (MNRPC) Zacharia Mtigandi amesema waliamua kuchagua kundi hilo kwa kuwa linapitia vikwazo vingi vya uzazi na wengine wanabakwa ila hawajui waanzie wapi.

Mtigandi amesema baada ya kupata elimu hiyo watakuwa na uelewa wa kupata haki zao na kuepuka kufanyiwa ukatili.

Mmoja wa washiriki, Mariam Nicodemus amesema ameachwa na mume wake na ametelekezewa watoto na hamsaidii kitu chochote na hana uhuru wa kufanya jambo lolote kwani anamlinda kila anapokwenda na anamzuia kuabudu kanisani.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi (ACP) Maresone Mwakyoma alipoulizwa kwa simu kuhusu matukio hiyo, amesema polisi wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii.

Advertisement