Wanawake Afrika waweka mikakati ya kujikwamua

Muktasari:

  • Mtandao wa kuwasaidia wanawake wa Afrika kibiashara utakuwa daraja ya kuwawezesha kutafuta fursa za mitaji, mafunzo, masoko ya bidhaa na huduma wanazozitoa.

Dar es Salaam. Wanawake na vijana barani Afrika wametakiwa kuunganisha nguvu zao katika masuala mbalimbali, ili washiriki kikamilifu katika soko huru la Afrika linalolenga kuwakwamua kiuchumi.

Rai hiyo imetolewa jana Alhamisi Novemba 30, jijini hapa na  Rais wa Mtandao wa Wanawake na Vijana Afrika - AfCFTA  (AWNA), Marry Charm wakati akizindua mtandao huo hapa nchini.

Amesema lengo la mtandao huo ni kumkomboa mwananchi na kijana kutoka kwenye ujasiriamali mdogo hadi kufikia hatua kubwa zaidi, ambayo itatengeneza ajira kwa watu wengine na kukuza pato la mtu mmojammoja na Taifa.

“Tunalenga kukata minyororo ya umasikini kwa wanawake na vijana, makundi haya mtakubaliana nami kwa muda mrefu yamekuwa nyuma iwe kielimu, kibiashara na kushirikishwa katika masuala mbalimbali, kimsingi yanahitaji kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ili kujikomboa na umasikini” amesema

Amesema miongoni mwa mambo wanayofanya ni kutoa mafunzo ya ujasiriamali, elimu ya masuala ya sheria na kanuni za kibiashara katika mataifa wanachama waliosaini na waliokubali kuingia kwenye mkataba wa soko huru la Afrika.

“Tunahitaji kuboresha namna ya kufanya biashara zetu kuanzia kwenye uzalishaji, ufungaji na masoko. Tunahitaji sheria zitakazoweka ushindani unaowiana kati ya nchi na nchi ili  kuondoa vikwazo” amesema.

Amesema Mtandao huo,  unalenga kuwaweka pamoja wanawake wa Afrika kibiashara iwe kwa wanaofanya biashara au wanaotoa huduma, ili kufaidi fursa na nafuu zilizotolewa na nchi wanachama.

Naye mmoja wa vijana aliyetoa mada kwenye hafla ya uzinduzi wa AWNA Tanzania, Gilbert Waigama amesema tafiti mbalimbali zimefanyika na imeonekana nchi za Afrika zinafanya biashara zaidi na mataifa yaliyo nje ya bara hilo, hivyo zinapeleka mitaji na fedha badala kushirikiana.

Amesema biashara zinazofanywa kati ya mataifa ya Afrika yenyewe kwa yenyewe mapato yake hayazidi asilimia 15 kulinganisha na yanavyofanya na mataifa nje ya bara hilo.

“Wakati umefika kwa wazalishaji Afrika kuzalisha bidhaa zenye ubora ili zinunuliwe ndani ya bara lao na kubakisha mitaji, kukuza ajira na teknolojia, tupunguze kuagiza bidhaa nje ya bara hili.” Amesema.

Amesema kuwa nchi za Afrika zimejiwekea malengo hadi ifikapo 2063 ziwe na uwezo wa kuzalisha bidhaa zao zitakazolitosheleza bara lao na nyingine kupeleka nje.

Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake na Vijana Afrika - AfCFTA  (AWNA) Tanzania, Bibie Msumi amewaasa wanawake kujitokeza na kujiunga na mtandao huo ili sauti zao zisikike na matatizo yanayowakabili yatatuliwe

Amesema kwa muda mrefu uamuzi kuhusu wanawake na vijana umekuwa ukifanywa bila kushirikishwa, hivyo ni wakati wao kushiriki mikutano na vikao kupitia Mtandao wao.

“Mtandao wetu ni fursa adhimu, nawaomba wanawake na vijana kushiriki kikamilifu ili tujikwamue kiuchumi” amesema.

Naye Ofisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Janeth Kafuko amesema ni vema wafanyabiashara wakawa mstari wa mbele kutoa taarifa wanapoombwa rushwa kwa ajili ya kupitisha bidhaa zao au kuingia mikataba.

“Tusitafute mteremko na urahisi wa kuingiza au kutoa bidhaa zetu, tufuate sheria za ndani na nje ya nchi. Wakati mwingine rushwa ndiyo inayofanya bidhaa zetu zipenye soko la kimataifa na hivyo maendeleo kusuasua” amesema.