Wanawake watetezi wa haki za binadamu wataka sera inayowalinda

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa, wanawake  wamekuwa wakikumbana na vitendo vya udhalilishaji wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kupigania haki.

Dar es Salaam. Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, wanawake watetezi wa haki za binadamu nchini wameshauri kuwepo kwa sera itakayowalinda wanawake watetezi ili wafanye kazi hiyo katika hali ya usalama.

Wito huo umetolewa leo Machi 8, 2024 na Ofisa Programu, Utafiti, Uchechemuzi na Uhusiano kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Nuru Maro kwenye mjadala wa wanawake watetezi wa haki za binadamu uliohusisha wakurugenzi wa mashirika  ya kutetea haki za binadamu.

Nuru amesema katika ufanyaji kazi wa wanawake hao, wanakumbana na changamoto nyingi ikiwamo kujeruhiwa, kudhalilishwa na kutolewa lugha chafu lakini hakuna sera inayowazungumzia kuwalinda wakati wakitekeleza majukumu yao.

“Kutokana na masaibu tunayokutana nayo katika kuwatafutia wananchi haki zao, tunaona ni wakati sasa nchi kuwa na sera itakayomlinda mtetezi wa haki, jambo ambalo halitatusaidia sisi tu bali kuwafikia wananchi wengi zaidi,” amesema ofisa huyo.

Akizungumza kuhusu mkutano huo, Nuru Maro amesema umewakutanisha wakurugenzi wa zaidi ya mashirika 50 na kujadili mada ya “Wekeza kwa wanawake, harakisha maendeleo,” ambayo ndio kaulimbiu ya siku ya wanawake mwaka huu inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka.

Amesema wamefanya hivyo wakiamini bila kuwekeza katika mashirika hayo na miradi ya maendeleo wanayoyafanya, wanawake hawawezi kufikia katika maendeleo.

“Kwa sababu kupitia taasisi zao wameweza kuwekeza miradi mbalimbali ikiwamo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii, lengo likiwa kuwakomboa wanawake na kuhakikisha dunia inakuwa  sehemu ya usalama kwa watu wote.

Amezitaja mada ambazo zimejadiliwa katika mkutano huo eneo la uwekezaji wa miradi ya wanawake, masuala ya tabianchi ambayo huwaathiri wanawake moja kwa moja na maeneo ya haki za kiuchumi.

 Mratibu wa Mtandao wa Wanawake Watetezi Tanzania(CWHRD),  Hilda Dadu amesema miaka 60 katika suala la haki za binadamu, Tanzania imepiga hatua akiwamo wanawake kushika nyadhifa mbalimbali, haki za afya.

Hilda amesema kupitia mashirika hayo ya haki za binadamu, katika tathimini yao wanaona wanawake wengi kwa sasa wanatambua haki zao na hivyo kusaidia kuzidai.

“Ukiacha wanawake kutambua haki zao, Serikali inahakikisha kwa namna moja au nyingine watu wanazipata haki hizo ikiwamo wanawake kumiliki mali, kufanya biashara jambo ambalo miaka ya nyuma ilikuwa ngumu,” amesema Hilda.

Mwanaharakati wa siku nyingi, Mary Rusimbi akichangia mada, amesema sasa ni wakati wa mashirika yanayojishughulisha na wanawake kukutana na viongozi wa taasisi mbalimbali kujua fedha zinazotengwa kwa ajili ya wanawake zinakwenda wapi.

“Hili litasaidia fedha hizo kuwafikia wanawake moja kwa moja, lakini kuyawezesha mashirika kufanya kazi zao badala ya kutegemea za wahisani kutoka nje ambazo wengi kwa sasa wanakuja na masharti yao na mengine ni magumu kutekelezeka kutokana na mila na desturi za nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Sofia Komba amesema bado kuna kazi kubwa ya kufanya tangu kupitishwa kwa azimio la Beijing.

Amesema tangu kuanza kwa harakati za kuleta usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume, kumekuwa na dhana potofu kuwa harakati hizo zimelenga kumfanya mwanamke afanane kila kitu na mwanamume, jambo ambalo sio kweli.

“Jamii katika hili inapaswa kujua azimio lililenga zaidi katika utendaji sawa wa kazi na mgawanyo sawa wa rasilimali huku suala la baiolojia ikiwamo kuzaa litabaki kuwa la mwanamke,” amesema Sofia.