Wanawake wawashangaa wanaume wanaobet, pool table

Muktasari:
- Wakati kundi la vijana wakijiingiza katika michezo ya kubahatisha na kamali, wanawake wao wamejikita kwenye shughuli ndogondogo za uzalishaji mali, hali ambayo imewafanya waanze kumiliki Uchumi ukilinganisha na wanaume wengi.
Songwe. Wakati kundi la vijana wakijiingiza katika michezo ya kubahatisha na kamali, wanawake wao wamejikita kwenye shughuli ndogondogo za uzalishaji mali, hali ambayo imewafanya waanze kumiliki Uchumi ukilinganisha na wanaume wengi.
Mwananchi imezungumza na baadhi wanawake katika maeneo mbalimbali mkoani Songwe ambao wanajishughulisha na biashara ndogondogo wamesema sasa wameamka na kujikita katika kufanya shughuli nyingi za kuichumi zinazowapatia kipato cha uhakika kila siku.
"Miaka ya nyuma tuliamini kuwa mwanamke ni mtu wa kukaa nyumbani akisubiri kuletewa na mume, lakini sasa tunajishughulisha wenyewe na hata kupata kipato cha kulea familia," amesema Amina Kyamba.
"Ukilinganisha na wanaume ambao wanachagua zaidi kazi za heshima ambazo pia hazipo sisi tunajikita kwenye shughuli ndogo za mahitaji ya lazima ya mwanadamu," ameongeza Amina.
Rose Mwashibanda amesema wanaume wengi na hasa vijana na wasomi wanachagua kazi wakijikuta wanaambulia patupu huku wakishinda kucheza bao, pool table, na kubeti (mchezo wa kubahatisha) huku wakikosa uhakika wa kupata kipato.
Amesema baadhi ya shughuli wanazofanya wanawake hivi sasa ni pamoja na kuuza matunda, karanga, bogamboga na shughuli nyingine za uzalishaji mali huku mitaji wakizungusha kupitia michezo ya upatu ya kuchangiana na vikoba.
Aidha wakati wanawake wakiwa vinala kumiliki uchumi kwa upande wa wanaume baadhi yao wamejiingiza katika shughuli za kuendesha pikipiki na bajaji huku waliowengi wangali katika hali ya kutojua cha kufanya hali ambayo imewafanya kujiingiza katika ulevi wa kupindukia.
Anna Julius mkazi wa Vwawa ambaye ni mjane na muuza maparachichi katika stendi ya Vwawa, amesema kupitia shughuli yake hiyo ameweza kupata mafanikio kadhaa ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba yake ndogo anayoishi na familia yake lakini pia anamudu kusomesha watoto wake kwa kuwapatia mahitaji muhimu.
"Unajua kazi ni kazi sisi hapa tunashinda juani ili kujishughulisha na ujasiriamali huu mdogo ambao unatupatia kipato cha uhakika kila siku. Haipiti siku sijaingiza hela, nacheza mchezo wa kila siku Sh5000 ambazo ninapopata gawio zamu yangu ikifika inakuwa hela kubwa ambayo naipeleka kwenye malengo yangu mengine," anasema Anna Julius
Baadhi ya vijana waliozungumza na gazeti hili wamekiri kuzidiwa na wanawake kiuchumi kutokana na mazingira ya maisha waliyo nayo ambapo shughuli nyingi za uchumi zimeshikwa na wanawake.
Moses Sikanyika amesema sababu inayowafanya vijana wa kiune kubweteka ni pamoja na kutegemea kuajiriwa na hasa wanapokuwa wamehitimu vyuo ambapo wakati wanasubiria ajira, wanajiingiza kucheza michezo ya kubahatisha ambayo pia haina uhakika.
Ofisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Mbozi, Noelia Kwai amekiri vikundi vya wanawake vinafanya vizuri ukilinganisha na vikundi vya vijana ambavyo hata vikipatiwa mkopo vinashindwa kurejesha lakini hali ni tofauti kwa vikundi vya wanawake vinafanya vizuri zaidi.
"Tunajitahidi kutoa elimu ya ujasiriamali lakini mapokeo yamekuwa kwa wanawake zaidi, tumefanya jitihada kutaka kuunda vikundi vya vijana lakini mwitikio wake ni mdogo," amesema Kwai.
Kwai ameongeza kuwa utafiti walionao ni kuwa vijana wengi hawaaminiani kwani chanzo cha kushindwa kurejesha mikopo ni baadhi yao kukimbia na fedha ingawa hali imekuwa tofauti kwenye mikopo ya pikipiki na bajaji waliopewa wanajitahidi kurejesha.