Wanazuoni wa habari kujadili mustakabali wa sekta hiyo Afrika

Muktasari:

  • Kongamano litafanyika Agosti 28 hadi 29, 2024 katika ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Dar es Salaam. Wakati sekta ya habari na mawasiliano ikiendelea kushuhudia mabadiliko makubwa yanayochangiwa na kukua kwa matumizi ya teknolojia, wanazuoni wa sekta hiyo kutoka maeneo mbalimbali duniani wanatarajiwa kukutana Tanzania kujadili mustakabali wa sekta hiyo.

Kongamano la wanazuoni wa mawasiliano Afrika Mashariki (EACA) linatarajiwa kufanyika Agosti 28 hadi 29, 2024 katika ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) chini ya mwenyeji wa mwaka huu, Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC).

“Kongamano hili linatumika kama jukwaa muhimu kwa wanazuoni, watafiti na watendaji wa sekta ya mawasiliano na vyombo vya habari katika nchi za Afrika Mashariki, barani Afrika na kwingineko duniani kukutana, kubadilishana uzoefu, kukuza ushirikiano unaochangia maendeleo katika sekta kwa ujumla,” amesema Amidi wa SJMC, Dk Mona Mwakalinga.

Amesema wageni zaidi ya 300 kutoka mataifa mbalimbali, yakiwemo ya Ulaya na Asia wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo ambalo litakuwa na mada kuu isemayo ‘Afrika na mjadala wa kimataifa kuhusu mawasiliano na vyombo vya habari.’

“Wanataaluma, watafiti, wahariri, wamiliki wa vyombo vya habari, wanahabari na hata maofisa wa Serikali na taasisi binafsi watahudhuria kongamano hili la kimataifa, ikiwa ni fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu kuhusu maendeleo kwenye taaluma ya habari,” amesema.

Amesema kongamano hilo la 14 la EACA litajumuisha pamoja na mambo mengine, hotuba mahususi, mijadala ya jopo, mawasilisho na ripoti za utafiti, yote yakilenga kuangazia nafasi za mawasiliano na vyombo vya habari katika maendeleo ya Afrika katika muktadha wa kimataifa.

Mratibu wa kongamano hilo kwa mwaka 2024, Dk Egbert Mkoko, amesema hii ni mara ya pili kwa kongamano hilo kufanyika nchini, akisisitiza juu ya umuhimu wake katika kuunganisha utafiti wa kitaaluma na uzoefu wa sekta.

Dk Mkoko ambaye ni mhadhiri wa SJMC, amesema mbali na mada kuu, kutakuwa na mada ndogondogo zihusuzo habari za uchunguzi na namna ambavyo kuibuka kwa teknolojia ya akili bandia kunaweza kuathiri sekta.

“Mada nyingine ambayo ni kivutio cha wengi ni hatima ya matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mawasiliano ya mataifa ya Afrika, hii tayari watu kutoka mataifa mbalimbali, ikiwemo Afrika Kusini wameomba kuifanyia wasilisho,” amesema Dk Mkoko.

Ametoa wito na kukaribisha wadau wote wa sekta ya habari na mawasiliano kuandaa ikisiri kwa ajili ya uwasilishaji wa mada wakati wa kongamano hilo.