Wanne wadakwa na pembe za ndovu

Muktasari:

  • Kamanda wa polisi mkoani Dodoma, Gilles Muroto, amewaeleza waandishi wa habari leo Februari 23, 2018 kuwa tukio hilo lilitokea Februari 20, 2018 wilayani Kondoa ambako watuhumiwa walikuwa katika harakati za mauziano.

Polisi mkoani Dodoma inawashikilia watu 16, wanne kati yao walikamatwa na vipande vinne vya pembe ya ndovu yenye uzito wa kilo 2.450 na thamani ya Sh67.6 milioni.

Kamanda wa polisi mkoani Dodoma, Gilles Muroto, amewaeleza waandishi wa habari leo Februari 23, 2018 kuwa tukio hilo lilitokea Februari 20, 2018 wilayani Kondoa ambako watuhumiwa walikuwa katika harakati za mauziano.

Muroto amewataja watuhumiwa ni wafanyabiashara wawili walioongozana na waendesha bodaboda wote wakazi wa Wilaya ya Chemba mkoani hapa.

“Watuhumiwa hao pia walikamatwa wakiwa na pikipiki mbili aina ya Fekon ambazo zinachunguzwa,  walipozingirwa na polisi walianza kuwatishia kwa visu wakitaka kukimbia kabla ya kutishiwa kwa risasi hewani na polisi,” amesema Muroto.

Katika tukio jingine, polisi wamewakamata watu watatu kwa kosa la kumiliki silaha kinyume cha sheria Februari 18,2018 katika kijiji cha Ilangali wilayani Chamwino.

Pia, wengine watatu wanashikiliwa kwa kosa la kumiliki bunduki tatu aina ya gobole ambazo walikuwa wanazitumia kwa uwindaji haramu katika mapori ya Mpwayungu yalipo ndani ya Hifadhi ya Ruaha.