Wanne wafa, 35 wajeruhiwa ajali ya basi Songwe

Muktasari:
Watu wanne wamefariki na wengine 35 wemejeruhiwa baada ya basi la Kilimanjaro Express kupata ajali eneo la Senjele wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe.
Songwe. Watu wanne wamefariki na wengine 35 wemejeruhiwa baada ya basi la Kilimanjaro Express kupata ajali eneo la Senjele wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe.
Basi hilo ambalo lilikuwa linatoka Tunduma kwenda Dar es Salaam limepata ajali leo Jumatatu Machi 14, 2022 asubuhi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Rashid Ngonyani amesema kuwa watu hao wanne wamefariki dunia papohapo na wengine 35 wakijeruhiwa.
Amesema kuwa majeruhi wamepelekwa hospitali kupata matibabu huku miili ya marehemu ikihifadhiwa katika hospitali ya Vwawa.
"Basi hilo limetumbukia kwenye korongo baada kuviringika mara kadhaa na hatimaye bodi ya gari kukatika kuanzia kwenye usawa wa madirisha" amesema Ngonyani
Kamanda Ngonyani amesema kuhusu chanzo cha ajali atatoa taarifa hiyo baada ya kukamilika kwa uchunguzi.
Ajali hiyo inatokea siku chache baada ya watu watatu kufariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa katika ajali nyingine iliyohusisha lori la mafuta na gari dogo kuungua baada ya kugongana eneo la Vwawa Mbozi.