Wanne wafariki dunia, watano walazwa kwa kipindupindu Kagera

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa akifafanua jambo wakati wa mkutano wa waandishi wa habari mjini Bukoba alipokuwa akitangaza mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindi ambao tayari umesababisha vifo vya watu wanne wilayani Misenyi. Picha na Alodia Dominick

Muktasari:

  • Watu wnne wamefariki dunia kwa ugnjwa kipindupindu uliolipuka katika Kijiji cha Buchurago Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera tangu Novemba 29, 2023.

Bukoba. Watu wanne wamefariki dunia na wengine watano wamelazwa kwa matibabu baada ya kutokea mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika Kijiji cha Buchurago Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa ametangaza kutokea kwa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika mjini Bukoba leo Desemba 4, 2023.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mlipuko wa ugonjwa huo umegundulika tangu Novemba 29, 2023 katika Kijiji cha Buchurago, Kata ya Bugorola Wilaya ya Misenyi.

"Mlipuko huo umebainika Novemba 29, 2023 katika kijiji cha Buchurago baada ya watu wawili kutoka nchi jirani ya Uganda kuingia kijijini hapo….hadi sasa, watu wanne wamefariki dunia na wengine watano wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Kajunguti wilayani Misenyi,’’ amesema Mwassa

Mkuu huyo amewataka wananchi mkoani Kagera kuchukua tahadhari kwa kuchemsha maji ya kunywa, kunawa mikono vizuri kwa sabuni, kuosha matunda kabla ya kula na kuepukana mikusanyiko isiyo ya lazima.

Savera Mutimavu, mkazi wa Manispaa ya Bukoba ameiomba Serikali siyo tu itoe elimu kwa umma kuhusu kujikinga dhidi ya ugonjwa huo, bali pia ihakikishe inawaweka katika hali ya tahadhari wataalam wa afya ili kukabiliana na milipuko katia maeneo mengine ndani na nje ya Mkoa wa Kagera kutokana na muingiliano uliopo.

‘’Serikali ihakikishe dawa, vifaa tiba na wataalam wanapatikana kwa haraka kulingana na mahitaji yanayojitokeza,’’ amesema Halima Said, mkazi wa Hamugembe, Manispaa ya Bukoba