Tanzania hupoteza Sh5.6 trilioni kila mwaka kwa kujisaidia vichakani

Muktasari:

  • Wakati hali duni ya vyoo ikitajwa kuwa na athari kubwa kwa ustawi wa jamii kiafya, kielimu na kijamii, Tanzania imetajwa kupoteza takribani Sh5.6 Trilioni kila mwaka kutokana na gharama za matibabu zinazosababishwa na hali duni ya huduma za maji na vyoo.

Dar es Salaam. Tanzania inakadiriwa kupoteza takribani Sh5.6 trilioni kila mwaka kutokana na gharama za matibabu ya magonjwa, muda wa uzalishaji mali kupotea kwa sababu ya kuuguza au kuugua magonjwa yanayotokana na kujisaidia nje.

Kwa mujibu wa Taarifa ya hali ya uchumi iliyotolewa na Benki ya Dunia (Tanzania Economic Update) ya mwaka 2023 imeonesha hiyo ni gharama ambayo nchi imekuwa ikiipata kutokana na hali duni ya huduma za maji na vyoo.

Hayo yamesemwa jana Jumapili, Novemba 19, 2023 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipotoa tamko kuhusu Siku ya Choo duniani huku akihamasisha jamii juu ya umuhimu wa matumizi ya choo bora kama njia muhimu ya kudhibiti magonjwa yatokanayo na kinyesi cha binadamu.

"Tunapoteza fedha nyingi, ambazo zingeweza kutumika katika shughuli zingine za maendeleo kama vile kuboresha miundombinu ya elimu, barabara, maji, mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, pembejeo za kilimo na mengine muhimu," amesema.

Waziri Ummy amesema hali duni ya vyoo ina athari kubwa kwa ustawi wa jamii kiafya, kielimu na kiuchumi.

"Taarifa ya Viashiria vya Afya ya mwaka 2022 inaonesha bado kuna asilimia 30 ya udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano. Hali hiyo pamoja na mambo mengine, inachangiwa na kukosekana kwa vyoo bora ambayo husababisha  watoto kupata magonjwa yatokanayo na kuhara na hivyo mwili kupoteza virutubisho," amesema.

Amesema wa mujibu wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia SDG 2030, lengo la 6.2 nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zinatakiwa kuhakikisha watu wote wanatumia vyoo bora na salama yaani ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo amesema ni Mkoa wa Dar es Salaam pekee ndiyo unaoongoza kwa sasa wa kuwa na kaya zenye vyoo bora kwa asilimia 98.5 ikifuatiwa na Ruvuma yenye asilimia 92.1 na Njombe yenye asilimia 87.6.

Amesema takwimu za hivi punde kupitia Ripoti ya Tafiti ya Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria ya Mwaka 2022 iliyotolewa na NBS imeonyesha kuna ongezeko kubwa la watu wanao tumia vyoo bora kutoka asilimia 21 mwaka 2016 hadi asilimia 74.8 mwaka 2022 alizozitaja kuwa ni hatua chanya katika kufikia lengo.

"Licha ya kuwa tumepiga hatua kwenye kiashiria hicho, bado kuna baadhi ya watu hawatumii vyoo ambapo takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 9.8 ya watu nchini hawana vyoo kabisa ambapo hali ni mbaya zaidi maeneo ya vijijini.

"Kwa mujibu wa taarifa hii asilimia 13.4 ya wakazi wa vijijini hawana vyoo kabisa. Tafsiri ya kiashiria hiki ni kwamba watu hawa ndiyo wanaojisaidia hovyo vichakani na maeneo mengine ambayo sio rasmi," amesema.

Amesisitiza kuwa hali hiyo inachangia kuwepo kwa magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu ambapo kwa kipindi cha Januari hadi Oktoba 2023 jumla ya watu 749 waliugua na 16 walipoteza maisha.

"Mikoa inayoongoza kwa kutokuwa na vyoo ni Katavi kwa asilimia 24.3, Simiyu asilimia 24.3 na Manyara 22.3 kufuatia takwimu hizi,  ninaziagiza Sekretatarieti za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha kaya zote nchini zinakuwa na vyoo bora," amesema.

Waziri Ummy ametoa rai kwa jamii kuendelea kuboresha vyoo vyao kuwa kwenye hali ya ubora huku akitoa angalizo kwa wale ambao vyoo vyao havijafunikwa na mapaa, wanaotapisha ili kujilinda na magonjwa katika msimu huu wa mvua nyingi.

"Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini imetoa tahadhari ya kuwepo kwa mvua kubwa za El-nino niikumbushe jamii yote kuhakikisha inakuwa na miundombinu imara ya vyoo ili kuhimili mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha.

"Ili kuepukana na hali hii ni vyema vyoo vikaboreshwa kwa kujenga mashimo imara na vilevile kutenganisha jengo la choo na shimo kwa lengo la kupunguza uzito wa jengo juu ya shimo la choo," amesisitiza.

Serikali inatekeleza Programu ya Huduma Endelevu ya Maji na Usafi wa Mazingira vijijini kwa kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu bora ya vyoo katika ngazi ya kaya, shule na vituo vya kutolea huduma za afya.

Mpaka sasa imeboresha miundombinu ya vyoo kwenye shule 1,283 kati ya shule 8,937 na vituo vya kutolea huduma za afya vipatavyo 1,902 kati ya vituo 5,625 vilivyopo kwenye Halmashauri za Wilaya pamoja na kuendeleza uboreshaji wa hali ya vyoo kwenye taasisi za umma.