Wapiga debe 30 wakamatwa Stendi ya Magufuli

Friday February 26 2021
usafiripic
By Fortune Francis

Dar es Salaam.  Wapiga debe 30 wamekamatwa katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli kilichozinduliwa siku mbili zilizopita na Rais John Magufuli.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Februari 26,2021 Meneja wa kituo hicho, Maira Mkama amesema wapiga debe waliokuwa Ubungo, Riverside na Mbezi wamevamia na kusababisha usumbufu kwa abiria.

"Leo tumeanza operesheni ya kuwakamata, hadi kufikia saa nne tumewakamata wapiga debe zaidi ya 30 na hapa Mbezi palikuwa na wapiga debe zaidi ya 100 bado waliokuwa Ubungo na wengine Riveside wote waliposikia kinafunguliwa wamevamia huku ndani,"amesema

Mkama amesema wameliomba Jeshi la polisi Kanda Maalum kuongeza askari na gari kwaajili ya doria ili kuwakamata wapiga debe watakaoendelea na shughuli hiyo.

Amesema wapiga debe hao wanasababisha usumbufu kwa abiri pamoja na kuhatarisha usalama wao hivyo viongozi wa kituo hicho watashirikiana na wamiliki wa mabasi kuangalia hatua za kuzichukua ili kuwaondoa wapiga debe.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua) Maulid Masalu amesema wanaweza kutoa ushauri lakini Serikali ndiyo yenye mkakati wa kuwaondoa wapigadebe.

Advertisement

"Hawa wapigadebe hawapo ndani ya stendi hii tu, wapo kuanzia stendi ya daladala wakati abiria anaposhushwa wanamvamia na kusababaisha usalama wake kuwa ndogo,"amesema Masalu.

Advertisement