Warioba afichua uteuzi wa Dk Salim ulivyopigwa vita

Waziri Mkuu na Jaji mstaafu, Joseph Warioba.

Muktasari:

  • Wakati Waziri Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim akizindua leo tovuti yake ya kumbukumbu alizokuwa akitunza, Jaji mstaafu Joseph Warioba amesena uteuzi wake wa kuwa waziri mkuu ulikuwa unapingwa.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu na Jaji mstaafu, Joseph Warioba amesema mwaka 1984 Rais wa Awamu ya Kwanza Hayati, Julius Nyerere alipomteua Dk Salim Ahmed Salim kuwa waziri mkuu kulikuwa na viongozi wengi waliopinga.

 Warioba amesema viongozi hao walipinga uteuzi kwa kile walichoeleza kuwa amekaa nje ya nchi kwa muda mrefu na hajui matatizo ya nchi hivyo atawezaje kusukuma maendeleo.

Ametoa kauli hiyo leo, Septemba 30, 2023 katika hafla ya uzinduzi wa tovuti ya Dk Salim ya hifadhi ya nyaraka zake.

Warioba amesema Nyerere hakujali maneno hayo kwani alikuwa anajua uwezo wa Dk Salim ndiyo maana alimteua.

“Alipokuwa waziri mkuu aliwashangaza wengi kwani alijifunza kwa muda mfupi kupitia kuzunguka nchi nzima na kuelewa matatizo. Alipofika sehemu na kukuta tatizo ambalo ni la utendaji halihitaji sera akitoka huko alitoa maelekezo huko nini kifanyike,” amesema Warioba.

Akitolea mfano wa ziara aliyofanya Lindi na Mtwara na kukuta matatizo mengi ikiwemo ya kukosekana kwa mavazi, watu wakivaa kama magunia lilimfanya kuagiza nguo zitafutwe na zipelekwe.

“Alikuwa ni mtu si wa maneno na vitendo pia. Miezi 18 ya uwaziri mkuu wake matokeo yake yalikuwa ni makubwa, ni mtu anayetunza kumbukumbu zake mahali popote hata katika mazungumzo kwenye vikao anaandika,” amesema Warioba.

Warioba amesema pia Dk Salim ni mtu aliyejifunza maisha yake yote, anasoma sana vitabu magazeti na ikiwa mtu amefika ofisini kwake atakuta rundo la magazeti ya ndani na nje na hufuatilia taarifa za habari muda unapofika za ndani na nje.

“Hiyo inamfanya hata anapotoa hoja anakuwa na uhakika anachosema na atasema kwa ufasaha bila kutazama uso wa mtu, haogopi na hatazami huyu ni mtu wa aina gani,” amesema Warioba.

Balozi mstaafu, Christopher Liundi amesema Dk Salim aliishi umajumui wake vyema huku akimuelezea kuwa wakati wote alikuwa mwenye harakati, akiwa kwenda mkutano ataandika vitu vya muhimu na taarifa zote alikuwa anaandika.

“Ni mtu mwenye uwezo wa kuwashirikisha watu na kuwaratibu, alikuwa na uwezo wa lugha, alikuwa na uwezo wa kusikiliza ukiwa na matatizo, maelezo atasikiliza na kujibu na ni ngumu kumuona amenuna pia ni mtu mwenye uwezo wa kujibu kutetea na kuelezea,” amesema Liundi.