Wasabato wafuturisha waumini wa Kiislamu kudhihirisha upendo
Muktasari:
Waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Nyanza wamewafuturisha waumini wa Dini ya Kiislamu Mkoa wa Shinyanga kama ishara ya mahusiano mema na ushirikiano kati ya waumini wa dini na madhehebu tofauti.
Shinyanga. Waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Nyanza wamewafuturisha waumini wa Dini ya Kiislamu Mkoa wa Shinyanga kama ishara ya mahusiano mema na ushirikiano kati ya waumini wa dini tofauti.
Akizungumza Aprili 18, 2023 mara baada ya futari hiyo, Mwenyekiti wa Jimbo la Nyanza, Askofu Enock Marwa Sando amesema hatua hiyo siyo tu unalenga kuimarisha na kudumisha mahusiano mema kati ya waumini wa dini na madhehebu tofauti, bali pia ni sehemu ya ibada kupitia matendo mema kwa wengine.
"Tumeungana na wenzetu Waislamu katika futari hii kama sehemu kumtafuta Mungu na kuomba kwa pamoja kwa ajili ya Mkoa wa Shinyanga na Taifa kwa ujumla,” amesema Askofu Sando
Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Makusanya amesema kitendo kilichofanywa na waumini wa Waadventista Wasabato ni ishara ya umoja wa kindugu kati ya waumini wa dini na madhhebu tofauti na unafaa kuigwa na wote wenye mapenzi mema.
"Kwa kweli nimefurahi sisi kukutana hapa tukifurahi bila kujali tofauti zetu kiimani; natamani kuona jambo hili la ushirikiano linaendelea hata katika nyanja na maeneo mengine. Huu ndio msingi wa umoja, upendo na mshikamano ambao ni moja ya sifa yetu Watanzania,” amesema Sheikh Makusanya
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Johari Samizi ameushukuru uongozi wa Kanisa la Wasabato kwa kuonyesha upendo kwa kwa waumini wa dini ya kiislamu na kushauri mahusiano hayo mema yaendelee hata baada ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Amewaomba viongozi wa dini mkoani Shinyanga kutumia nafasi na ushawishi wao kwa jamii kukemea na kupambana na vitendo vya ukatili na imani za kishirikina zinazosababisha mivutano ndani ya jamii.
"Watu wengi wamepungukiwa na hofu ya Mungu ndio maana tunashuhudia vitendo ambavyo baadhi vinakiuka maadili na tamaduni zetu; nawasihi viongozi wa dini watumie majukwaa yao kukemea vitendo hivyo,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.