Washikiliwa kwa kumshambulia waliomtuhumu kwa ugoni

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Mchomvu akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Februari 29,2024 ofisini kwake, Madema.

Muktasari:

  • Tukio hilo lilitokea baada ya Mundhir kumchukua mwanamke na kumpeleka nyumbani kwake, ambapo alivamiwa na watu watano. Wahalifu hao walimpora Mundhir simu na vitu vingine vya thamani. Jeshi la Polisi lilifanya msako na kuwakamata watuhumiwa, akiwemo Khamis Seif Khamis na mke wake

Unguja. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, linawashikilia watuhumiwa wawili waliojichukulia sheria mkononi kwa kumshambulia mwanaume mmoja kwa madai ya kutembea na mke wa mtu.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, Februari 29, 2024 na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Richard  Mchomvu wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Madema.

Amesema Mundhir Khamis Karama (32) mkazi wa Kijichi kisiwani hapa, alishambuliwa kwa fimbo na vitu vyenye ncha kali na kufungwa kitambaa usoni, baadaye kupelekwa sehemu kusikojulikana kwa kutumia usafiri wa gari aina ya Noah.

"Siku ya tukio Mundhir anadaiwa kumchukua mwanamke na kumpeleka nyumbani kwake huko Kijichi, baada ya muda mfupi wakiwa chumbani alivamiwa na watu watano ambao mmoja wao alidai kuwa mume wa mwanamke huyo," amesema Mchomvu

Mchomvu amesema wahalifu hao walimpora Mundhir simu aina ya Samsung yenye thamani ya Sh400,000,  na waleti yenye vitambulisho mbalimbali, pia walimtaka apige simu kwa ndugu zake atumiwe pesa ndipo aachiliwe"  Baada ya kushindwa kufanikiwa takwa hilo walimtelekeza  eneo la Mwanakwerekwe," amesema.


Amesema, baada ya tukio hilo kuripotiwa, Jeshi la Polisi lilifanya msako na kuwakamata watuhumiwa walioshiriki tukio hilo akiwemo Khamis Seif Khamis (30) na mke wake (Aliekutwa ndani ya chumba na Mundhir) na juhudi za kuwakamata wengine zinaendelea.

Wakati huohuo, jeshi hilo limepinga kuwepo kwa matukio ya kutekwa wananchi kwa kutumia mapanga, baada ya picha jongefu iliyosambaa katika mitandao ya kijamii na kuzua hofu kwa wananchi.

Kamanda Mchomvu amewataka wananchi kupuuza taarifa hizo kwani hazina ukweli, “huu ni uzushi, hakuna vikundi vya aina hiyo na tunaomba wananchi wapuuze taarifa hizo sio za kweli,"amesema.

Katika hatua nyengine, jeshi hilo limewakamata watuhumiwa wawili wanaodaiwa kuiba pikipiki aina ya TVS yenye  thamani ya Sh2.5 milioni, ikiwa ni mali ya Nassir Jamal Nassor (27) mkazi wa Fuoni Mambosasa.

Amesema mmiliki wa pikipiki baada ya kuibiwa aliwatuhumu baadhi ya watu na aliamua kuwakusanya madereva wa bodaboda wa kituo cha Fuoni Melitano ili kwenda kuwavamia wanaotuhumiwa na wizi huo.

Hivyo, amemkamata  Mundhir Mohd Khamis (20) na Saleh Mohd Mwinyi (20) wote wakaazi wa Fuoni.


Hata hivyo, Mchomvu amesema Mundhir Mohd Khamis aliwahi kufikishwa mahakamani kwa kosa la wizi, kesi namba 292/2023 na kesi hiyo iliondolewa kwa mashahidi kutofika kutoa ushahidi.

Sambamba na hayo, Mchomvu ametoa wito kwa wananchi kutojichukulia sheria mkononi, kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na hawawezi kufumbia macho matukio ya aina hiyo.

Mmoja kati ya wakazi wa Fuoni, Hawa Ismail Haji amesema kwa sasa jeshi hilo  linatakiwa kuimarisha ulinzi kwani hali iliyopo inatishia amani.