Sakata la fumanizi laibua mapya

Monday August 09 2021
fumanizi pc
By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Wakati mjadala wa sharti la cheti cha ndoa kwenye fumanizi ukishika kasi, imeelezwa kuwa zipo ndoa hazina vyeti na zinatambulika kisheria, lakini wengi hawana uelewa huo.

Hata hivyo, baadhi ya wanasheria wamewashauri watu badala ya kufumania, kufungua kesi ya madai na kumdai fidia kiasi chochote mtu mwenye uhusiano na mwenza wake.

Juzi, Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene alisema, “itahesabiwa fumanizi hadi pale huyo anayefumaniwa, iwe mwanamke au mwanamume awe na cheti cha ndoa halali. Sio mtu alikuwa rafiki yako kwa muda, wewe bado unatafuta uhalali wa kuonekana unammiliki, unamvamia na kurekodi picha kisha kusambaza.”

Soma hapa:Simbachawene: Watakaoandaa fumanizi kukamatwa

Kauli ya Simbachawene kuhusu cheti cha ndoa na fumanizi ilikuja baada ya kusambaa video mtandaoni inayoonyesha watu wakipigwa kwa madai ya kufumaniwa.

Hata hivyo, akizungumza na gazeti la Mwananchi jana, Wakili Bashir Yakub alisema ili uite fumanizi, lazima uwe na ndoa, lakini sio lazima uwe na cheti.

Advertisement

Mwanasheria huyo alisema kuna ndoa za kimila, za kuishi pamoja kwa zaidi ya miaka miwili hazina vyeti lakini zinatambulika kisheria. Alisema fumanizi linapaswa kufanywa na mwanandoa lakini sio lazima awe na cheti cha ndoa kwa kuwa Watanzania wengi hawana vyeti.

“Alichosema waziri ni kweli, ili uite fumanizi lazima uwe na ndoa, ila sio lazima uwe na cheti; kuna ndoa za kimila na za kuishi pamoja kwa zaidi ya miaka miwili, hizi zipo nyingi na hazina vyeti lakini zinatambulika kisheria,” alisema wakili Yakub.

“Tukirudi kwenye fumanizi, hili ni sawa kufanywa na mwenye ndoa, changamoto ni kwamba wengi hawajui sheria. Ukijiridhisha kuna mtu ana uhusiano na mke au mume wako na ushahidi upo, unaweza kumfungulia kesi ya madai ukadai fidia.”

Soma hapa: Auawa kwenye fumanizi

Yakub alisema wanaofumania wengi huishia kufanya jinai kwenye fumanizi wakati ingewezekana kufungua kesi ya madai na kumdai fidia kiasi chochote mtu mwenye uhusiano na mwenza wake. Kule haumshtaki mwenzi wako, bali yule ambaye ameingia naye kwenye mapenzi baada ya kuwa na ushahidi wa kutosha utafungua kesi ya kudai fidia, utadai kiasi utakachoona lakini wengi hawatumii fursa hii wanajikuta wao wakiangukia kwenye jinai,” alisema Yakub.

Akizungumzia vitendo vya kupanga fumanizi, Waziri Simbachawene alipiga marufuku vitendo hivyo vinavyohusisha udhalilishaji na ukatili kwa watu wawili walio faragha, akisema ni kinyume cha sheria.

“Hakuna fumanizi linaloweza kupangwa na kikundi kinachokwenda kuvamia na kuingilia uhuru wa watu walio kwenye faragha, kitendo hiki ni kinyume cha sheria. Hata pale inapokuwa fumanizi lazima lisiwe jambo la kupangwa na watu kuvamia mahali walipo wawili,” alisema Simbachawene. Alisema vitendo hivyo vinakiuka heshima na utu, hasa wa wanawake ambao ndio waathirika wakubwa wa mafumanizi hayo na kupangwa.

“Mtu umemkuta amekuingilia kwenye himaya yako, ustaarabu ni kwenda kumfungulia kesi mahakamani au kulalamika kituo cha polisi ili akamatwa, lakini huruhusiwi kumkamata mhalifu kwa kushirikiana na kikundi cha watu na kutoa adhabu.”

Waziri Simbachawene aliliagiza Jeshi la Polisi kufuatilia matukio hayo ya udhalilishaji yanapojitokeza na kuwakamata wahusika na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Advertisement