Washtakiwa watatu kesi ya mauaji ya askari Loliondo waachiwa huru

20 kortini madai ya mauaji

Muktasari:

Mwanafunzi wa Kidato cha Nne ni miongoni mwa watu watatu kati ya 27 waliofutiwa kesi mauaji ya askari polisi yaliyotokea kufuatia vurugu za kupinga mpango wa Serikali wa kuweka mipaka katika pori tengefu la Loliondo, wilayani Ngorongoro.

Arusha. Mwanafunzi wa Kidato cha Nne ni miongoni mwa watu watatu kati ya 27 waliofutiwa kesi mauaji ya askari polisi yaliyotokea kufuatia vurugu za kupinga mpango wa Serikali wa kuweka mipaka katika pori tengefu la Loliondo, wilayani Ngorongoro.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imewafutia kesi watu hao baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kueleza hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi ya watu hao.

Leo Julai 28, 2022, mahakama hiyo ilipanga kutoa uamuzi mdogo wa ombi la mawakili wa utetezi walioitaka mahakama hiyo isikilize na kutolea uamuzi shitaka la kula njama wakati upelelezi wa kesi ya mauaji ukiendelea ili wateja wao wapatiwe haki kwa wakati.

Kabla ya uamuzi huo haukusomwa, wakili wa Serikali Upendo Semkole alisimama na uitaarifu mahakama kuwa DPP hana nia ya kuendelea na mashatka dhidi ya watu hao akiwemo mwanafunzi wa shule ya sekondari, Simeli Parmwati ambaye alitakiwa kuwa amejiunga Kidato cha Tano.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Fadhil Mbelwa aliyeshika nafasi ya Hakimu Mkazi Harieth Mhenga ambaye ndiye anayesikiliza kesi hiyo, alibariki taarifa hiyo na kutamka kuwa washtakiwa huao wako huru.

Kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinampa DPP mamlaka ya kuachana na shitaka la jinai wakati wowote wa kesi kabla ya kusomwa hukumu.

Wengine walioachiwa ni Fred Ledidi ambaye kwa maelezo yaliyotolewa mahakama Julai 14, 2022, ni mwanafunzi anachukua shahada ya uzamivu (PhD), na alipaswa kuwasilisha maandiko yake ya kitaaluma kwa ajili ya kuendelea na masomo hayo.

Mwingine aliyeachiwa ni Lukerenga Koyee ambaye ilidaiwa mahakamani hapo kuwa ni mgonjwa wa figo.

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Ndirango Laizer.

Wengine ni Molongo Paschal, Albert Selembo, Lekayoko Parmwati, Sapati Parmwati, Ingoi Olkedenyi Kanjwel, Sangau Morongeti, Morijoi Parmati, Morongeti Meeki, Kambatai Lulu, Moloimet Yohana na Joel Clemes Lessonu.

Wapo pia Simon Orosikiria, Damian Rago Laiza, Mathew Eliakimu, Luka Kursas, Taleng'o Leshoko, Kijoolu Kakeya, Shengena Killel, Kelvin Shaso Nairoti, Wilsom  Kiling, James Taki, Simon Saitoti na Joseph Lukumay.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa mawili likiwamo la kula njama ya kufanya mauaji na shitaka la pili likiwa la mauaji.

Ilidaiwa kuwa kwa tarehe na sehemu isiyofahamika wilayani Ngorongoro, washtakiwa walipanga njama ya kuua maafisa wa Serikali na maafisa polisi watakaoshiriki zoezi la kuweka mipaka pori tengefu la Loliondo.

Ilidaiwa pia kuwa Juni 10, 2022 katika eneo la Ololosokwan, wilayani Ngorongoro, kwa nia ovu, washtakiwa hao walisababisha kifo Koplo Garlus Mwita.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 5, 2022.