Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasichana 1,600 waliokatisha masomo watambuliwa, kurudi shule

Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Zuwena Omary (wa tatu kulia), akiwa na Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Lindi, Bahati Meshack (kulia) pamoja na maofisa wa Taasisi ya Doris Mollel ambao ni Ofisa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Jacqueline Shuma (wa pili kulia), Ofisa Ulinzi, Bishagazi Selemani (kushoto) na Ofisa Rasilimali Watu na Uendeshaji, Beatrice Matama (wa pili kushoto), wakati wa hafla ya uzinduzi wa utekelezaji wa Mpango wa Afua za Ulinzi wa Kijamii kwa Wasichana Balehe na Wanawake Vijana (AGYW) mkoani Lindi.

Muktasari:

  • Lengo la mpango huo ni kuwasaidia wanufaika hao kurejea katika mfumo wa elimu pamoja na kuimarisha huduma za ulinzi kwa manusura wa ukatili wa kijinsia, ukatili dhidi ya watoto na biashara haramu ya binadamu.

Dar es Salaam. Zaidi ya wasichana 1,600 waliokatisha masomo wametambuliwa kunufaika na Mpango wa Afua za Ulinzi wa Kijamii kwa Wasichana Balehe na Wanawake Vijana (AGYW), unaolenga kuwawezesha kurejea katika mfumo wa elimu na kupata huduma za ulinzi wa kijamii.

Mpango huo unaofadhiliwa na Global Fund na kutekelezwa na Christian Social Services Commission (CSSC) kwa kushirikiana na Doris Mollel Foundation (DMF), unawalenga wasichana na wanawake vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 katika halmashauri 47 za mikoa 15 nchini.

Kupitia mpango huo, wasichana hao wanasaidiwa kurejea katika shule za kawaida, kujiunga na programu za Elimu Mbadala ya Msingi Tanzania (Cobet) na Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (Memkwa) au kupata mafunzo ya ufundi stadi.

Miongoni mwa faida wanazopata ni kulipiwa ada za shule, kupatiwa sare, vifaa vya kujifunzia na vifaa vya kujisitiri. Pia wasichana wanaokabiliwa na changamoto za umbali, ndoa za utotoni au shinikizo la kifamilia hupatiwa msaada wa malazi ya bweni, hosteli na usafiri ili waweze kuendelea na masomo.

Mbali na elimu, mpango huo umeimarisha huduma za ulinzi kwa manusura wa ukatili wa kijinsia, ukatili dhidi ya watoto na biashara haramu ya binadamu. Vituo vilivyochaguliwa vinatoa malazi ya dharura, ushauri wa kisaikolojia, huduma za afya na msaada wa kisheria.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Zuwena Omary, amepongeza utekelezaji wa mpango huo akisema unasaidia kutatua changamoto ya muda mrefu ya wasichana kushindwa kuendelea na masomo.

"Mpango huu unatatua hitaji ambalo tumekuwa tukilishuhudia likiongezeka kwa miaka mingi. Wasichana wetu wanastahili kupata msaada huu, na ninauomba uongozi wa mpango huu kuangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya wanufaika," amesema.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Caring Hands Loving Hearts Safe House katika Manispaa ya Lindi, Eveline Jumanne, amesema kituo hicho kipo tayari kushirikiana na mpango huo katika kutoa hifadhi na msaada kwa manusura wa ukatili.

Maofisa wa mpango huo wamesema ufuatiliaji wa maendeleo ya wanufaika utafanyika baada ya miezi mitatu na sita ili kutathmini maendeleo yao katika elimu pamoja na upatikanaji wa huduma za kinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).