Wasifu uteuzi wa Dk Nchimbi CCM, Chadema waonya

Muktasari:

Wanasiasa mbalimbali wamezungumzia uteuzi wa Dk Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wakimpongeza, huku Chadema  kikimtahadharisha katika nafasi hiyo mpya.

Dar es Salaam. Baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kumteua Dk Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu  Mkuu, wanasiasa wa chama hicho wamesifu uteuzi wake, huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikimtahadharisha na siasa za mabavu.

Dk Nchimbi ameteuliwa leo Jumatatu, Januari 15, 2024 na Kamati Kuu ya CCM na baadaye kuridhiwa na Halmashauri Kuu ya chama hicho, iliyoketi visiwani Zanzibar saa chache zilizopita na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Kuteuliwa kwa Dk Nchimbi kunakuja wiki sita tangu CCM ilipokosa Katibu Mkuu, baada ya aliyekuwa na wadhifa huo, Daniel Chongolo kujiuzulu kwa madai ya kuchafuliwa mitandaoni.

Uteuzi huo umewaibua wadau mbalimbali waliozungumza na Mwananchi Digital akiwemo Mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT), Sophia Simba aliyeeleza kufurahishwa na hilo.


Sophia Simba aliyewahi kuwa mbunge wa Viti Maalum amesema Dk Nchimbi ni mtu sahihi kwenye wadhifa huo kwa kuwa hana unafiki na ni muwazi.

Amesema CCM ilihitaji mtu kama Dk Nchimbi kwenye nafasi hiyo, huku akisisitiza kwamba anastahili kwa uzoefu na uwezo wake.

“Maa shaa Allah…sasa CCM tumepata Katibu Mkuu, anafaa kwa kuwa hana unafiki wala makundi na ni muwazi. Chama kilihitaji mtu kama yeye, sio hao wanaopitapita,” amesema.

Ikumbukwe Sophia ni mmoja wa wanasiasa waliowahi kukumbwa na adhabu pamoja na Dk Nchimbi baada ya kutuhumiwa kwa hujuma ndani ya CCM katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Katika uchaguzi huo, Dk Nchimbi alijitokeza hadharani kupinga uamuzi wa Kamati Kuu kumpendekeza Dk John Magufuli kuwa mgombea wake wa urais.

Dk Nchimbi, Adam Kimbisa na Sophia Simba walikuwa wanamuunga mkono Edward Lowassa aliyekuwa akiwania urais mwaka 2015 kupitia CCM kabla ya jina lake kukatwa na kutimkia Chadema.

Hata hivyo, baada ya mgombea urais kupatikana, Dk Nchimbi alijitokeza hadharani na kueleza kwamba kama chama kimefanya uamuzi, mtu akiendelea kuupinga, huo ni usaliti.

Kutokana na tuhuma hizo ambazo hatua zilichukuliwa mwaka 2017, Sophia alifukuzwa uanachama huku Dk Nchimbi akipewa onyo kali na kutoruhusiwa kugombea nafasi yoyote kwa miaka minne.

Mbali na Sophia mwingine aliyezungumzia uteuzi huo ni Balozi Christopher Liundi aliyesema Dk Nchimbi ni miongoni mwa wanasiasa wenye mizizi ndani ya chama hicho kwa kuwa walianza kukitumikia kitambo.

“Nakumbuka baba yake (Mzee John Nchimbi) alikuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kigoma, wakati huo mimi nikiwa mkuu wa mkoa huo, kwa hiyo Nchimbi alianza mbali sana na CCM,” alisema.

Kwa uzoefu wa Dk Nchimbi, Balozi Liundi aliyewahi kuiwakilisha Tanzania nchini Ethiopia, alisema utamwezesha kukiongoza chama hicho katika dira inayostahili na kupata manufaa makubwa kwa wanachama na Taifa kwa ujumla.

Aliongeza fani yake (Dk Nchimbi) katika diplomasia itampa nafasi ya pekee kutumia mbinu mbalimbali za kidiplomasia kutatua matatizo mbalimbali sio tu ya wanachama bali kitaifa.

“Nina matumaini makubwa wala sina mashaka lakini la msingi ni tumsaidie, pale ambapo utahitajika ushauri ashauriwe ili apate mafanikio mazuri kwenye kazi yake kubwa na manufaa makubwa kwa chama hicho na taifa kwa ujumla,” alisema Balozi Liundi aliyewahi pia


Chadema wamkaribisha kwa onyo

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania-Chadema chenyewe kimemkaribisha kwenye ulingo wa siasa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amemkaribisha Dk Nchimbi kwenye mapambano ya kisiasa huku akimtahadharisha na siasa za mabavu.

“Anapaswa kutambua kuwa amerithi nafasi katika chama ambacho kinaogopa mijadala ya wazi na maandamano, kwa hiyo ataamua awe hivyo au abadilike,” amesema Mrema alipozungumza na Mwananchi lililotaka kupata mtazamo w juu ya uteuzi huo wa Dk Nchimbi

Hata hivyo, Mrema amemtaka mtendaji mkuu huyo mpya wa CCM, ajiandae kukabiliana na ushindani wa hoja na sio kutumia nguvu ya dola.

“Akiamua kutumia nguvu ya dola na mabavu hatadumu kwa muda mrefu kwenye nafasi yake, kwa sababu duniani kote siasa za mabavu hazijawahi kushinda,” amesema Mrema.


Chongolo ampongeza

Wakati Chadema wakieleza hayo, katika ukurasa wake wa Instagram, aliyekuwa na wadhifa huo, Chongolo amempongeza Dk Nchimbi kwa kuaminiwa na kupewa nafasi hiyo, akisema hana mashaka naye.

“Hongera saaana Balozi Dk Emmanuel Nchimbi kwa kuaminiwa na Mwenyekiti wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan na kupendekeza jina lako na NEC kuridhia wewe kupeperusha bendera ya CCM kwa dhamana ya mtendaji mkuu.

“Imani ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwako ni kubwa sana nasi wana CCM hatuna mashaka nawe. Hongera sana na kila la kheri!” aliandika.