Wasifu wa Mwalimu Nyerere waandikwa kwa mara ya kwanza na Watanzania

Profesa Issa Shivji akizungumza wakati akichambua kitabu cha wasifu wa Mwalimu Nyerere kwenye mdahalo wa kitaifa kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwake unaofanyika katika chuo cha Uongozi Kibaha mkoani Pwani.

Muktasari:

Kwa mara ya kwanza waandishi wa Kitanzania wameandika kitabu cha wasifu wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza waandishi wa Kitanzania wameandika kitabu cha wasifu wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Aprili 9, 2022 na mwanazuoni Profesa Issa Shivji alipokuwa anachambua kitabu cha wasifu wa Mwalimu Nyerere kwenye mdahalo wa kitaifa kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwake unaofanyika katika chuo cha Uongozi Kibaha mkoani Pwani.

Profesa Shivji amesema wasifu zote za Mwalimu zilizowahi kuandikwa huko nyuma ziliandikwa na waandishi wa nchi za nje, lakini kwa mara ya kwanza wasifu huu wa sasa umeandikwa waandishi wa Tanzania.

“Wasifu zote zilikuwa zikiwandikwa na watu wa nje, lakini hivi sasa waandishi wa ndani tumeweza kuandika wasifu wa Hayati Baba wa Taifa wenyewe Watanzania.

“Pia shughuli haina mkono wa ufadhili wa watu kutoka nje bali umefadhiliwa na Tasisis ya kitanzania ambayo ni Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

🔴 #LIVE: MDAHALO WA KITAIFA KUADHIMISHA MIAKA 100 YA KUZALIWA MWALIMU NYERERE

“Hivyo hakuna hata senti moja tuliyoipokea wala kuomba kutoka kwa wafadhili wa nje au wa ndani,’amesema mwanazuini huyo.

Profesa Shivji amesema hata katika kukichapisha kitabu hiko, kimechapisha na shirika la Kitanzania la Mkuki na Nyota, kazi aliyokiri kwamba imefanywa kwa kiwango cha juu cha kimataifa na kuongeza kuwa wanafarijika kwa kutekeleza kwa vitendo falsafa ya Mwalimu Nyerere ya kujitegemea.

“Kama tujuavyo Mwalimu alikuwa akirudia rudia kusema kwamba ukiwa tegemezi utapoteza uhuru wako wa kujiamulia mambo yako mwenyewe, ukiwa tegemezi kama nchi utapoteza uhuru wako wa kujiamulia mambo ya yako, ukiwa tegemezi kama mtu utapoteza uhuru wako wa kutoa maoni yako .

“Nahisi jambo hili tukajifunza katika kuandika vitabu hivi, ambapo katika kuandika hakuna mtu yoyote wa Serikali wala chama aliyetuangilia kuandika mpaka kufikia hatua ya kuchapisha,”amesema Profesa Shivji.