Wasimulia Askofu Sendoro alivyovunja makundi Dayosisi ya Mwanga ilipozaliwa
Muktasari:
- Padri Nicolaus Ngowi aliyefariki dunia katika ajali ya gari juzi jioni atazikwa Jumatano ya Septemba 17, mwaka huu kwenye makaburi ya wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, yaliyopo Manyoni, mkoani Singida
Moshi. “Nguzo imeanguka,” hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya wachungaji wa Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT), kusimulia namna Askofu Chediel Sendoro alivyowaunganisha wanadayosisi hiyo na kuondoa makundi yaliyokuwa yakivutana na kusababisha migogoro.
Askofu Sendoro alifariki dunia Septemba 9, 2024 kwa ajali iliyotokea eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro saa 1:30 usiku, baada ya gari aina ya Toyota Prado alilokuwa akiliendesha kutokea Kileo kuelekea nyumbani Mwanga, kugongana uso kwa uso na lori.
Historia inaeleza kuwa, Askofu Sendoro ndiye alikuwa wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga na aliingia kazini Jumapili ya Novemba 6, 2016 ilipozaliwa dayosisi hiyo mpya baada ya kugawanywa dayosisi mama ya Pare.
Akimzungumzia Askofu Sendoro leo Jumatano Septemba 11, 2024 akiwa msibani, mchungaji kiongozi wa KKKT Usharika wa Mchali, Dayosisi ya Mwanga, Msifuni Luka amesema wamempoteza kiongozi aliyewatumikia.
Mchungaji Luka amesema katika kipindi cha mchakato wa kuanzishwa kwa Dayosisi ya Mwanga, kulijitokeza migogoro na mivutano iliyoleta mgawanyiko ndani ya kanisa.
Hata hivyo, amesema baada ya Sendoro kuchaguliwa kuwa askofu, alihimiza umoja na mshikamano na kuwatangazia ushirikiano ili kuwaunganisha waumini wote wa dayosisi hiyo.
"Askofu Sendoro amekuwa mtumishi ambaye ametumika kwa nguvu na uaminifu sana katika dayosisi hii, kwa kipindi ambacho ametumika, alikuwa mwenye upendo na ametusaidia kumaliza mivutano tuliyokuwa nayo na sasa tunafurahia umoja wetu,” amesema Mchungaji Luka.
Pia, amesema ni mtu aliyekuwa anapenda kuhimiza maisha ya umoja, upendo, mshikamano na kuepuka mifarakano.
“Alituunganisha pamoja baada ya kupitia kipindi cha migogoro kwa muda mrefu katika dayosisi hii," amesema Mchungaji Luka.
"Alikuwa mtu mwema sana, alituletea umoja na kuimarisha uhusiano na dayosisi yetu mama ya Pare. Alikuwa karibu na kila mtu na hata watoto walimfahamu kupitia matukio mbalimbali yaliyowaunganisha.”
“Alikuwa msikivu, akipokea ushauri kutoka kwa kila mtu kuanzia msharika wa kawaida, wachungaji, wainjilisti na wengine wote, naweza kusema mbuyu umeanguka, tumepoteza," amesema Mchungaji Luka.
Naye Mchungaji wa Usharika wa Mruma, Samson Mbwambo amesema Askofu Sendoro alikuwa kiungo kikubwa cha dayosisi yao kwa sababu alipokuwa akiingia kazini, alikuta tayari kuna makundi ya waumini ambayo hayaelewani.
"Kulikuwa na makundi mabaya wakati dayosisi hii inazaliwa, lakini aliingia na kauli mbiu yake aliyoiimba kuwa, ‘wote wawe na umoja’ na alitimiza kauli mbiu hiyo kwa vitendo,” amesema Mchungaji Mbwambo.
Amesema alileta ushirikiano kwa wachungaji, washarika na hata waliokuwa wanaharakati pia kuliwaunganisha.
Mchungaji Mbwambo amesema hali hiyo aliijenga pia hata kwa Dayosisi ya Pare, “hakika aikuwa kiungo kikubwa na Mungu alimtumia kutuleta pamoja kama watumishi katika kuitenda kazi yake tuliyoitiwa hapa duniani, hakudharau mtu, alithamini kila mtu na kuona kila mmoja ana mchango katika kutenda kazi ya Mungu.”
Amesema watamkumbuka kwa upendo wake, moyo wa kutumikia na jinsi alivyojitoa hasa kwa kutoa huduma ya kuihubiri injili ambayo kila mmoja anatamani angeendelea kuwepo.
“Lakini leo amelala kimya, hatuna budi kumshukuru Mungu na kulibeba hili,” amesema Mchungaji Mbwambo.
Mwanafunzi wa uchungaji, majirani wamlilia
Mtheolojia, Silvanus Msuya amesimulia namna Askofu Sendoro alivyomchukua kutoka Dar es Salaam na kumleta Mwanga kusomea uchungaji.
Msuya ambaye kwa sasa amemaliza masomo ya uchungaji katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, anasubiri kubarikiwa.
Amesema Askofu Sendoro alimtoa katika namna ambayo si njema na kumpeleka katika kumtumikia Mungu.
"Mipango ya Mungu hatuna uwezo wa kuhoji, lakini tumeupata msiba mkubwa na mzito sana katika dayosisi yetu ya Mwanga. Alikuwa mtu wa watu, mwenye upendo kwa watu wa aina zote. Binafsi, amenitoa katika hali isiyokuwa njema na kunileta kwenye njia ya kumtumikia Mungu akinionyesha upendo na kunikubali jinsi nilivyo. Niliishi Dar es Salaam, lakini mimi ni mkazi wa Mwanga na katika maisha unaweza kupitia matukio mbalimbali ya kawaida ya kibinadamu lakini baba huyu alinibeba akanilea na leo niko hivi nilivyo,” amesema Msuya.
Hata hivyo, amesema si kila mtu anapokutazama anaweza kuona utume uliopo ndani yako au wito wako, lakini Askofu Sendoro alibaini udhaifu aliokuwa nao na akabaini Mungu ameweka kitu ndani yake.
Amesema wakati waumini wa KKKT Mwanga na maeneo mengine wanapoomboleza kifo chake, wakumbuke kufuata nyayo zake kwa kuwa ni mengi mema na makuu amewaachia na hawana budi kuyarithi na kuyaendeleza ikiwamo umoja, upendo na mshikamano.
Onesta Mollel, mwalimu wa Shule ya Viziwi Mwanga ambaye pia ni jirani wa marehemu, amesema Askofu Sendoro alikuwa mlezi wa shule hiyo na aliwapenda sana watoto wenye ulemavu na kuwajali.
Adrin Msangi ambaye pia ni jirani yake, amesema; "kijumla msiba huu ni pigo kubwa hata kwetu sisi majirani, mbali ya kanisani kwake, alikuwa msaada mkubwa hata kwetu, tumeupokea huu msiba kwa masononeko makubwa, hakupenda makuu tulizoea kumuita baba mshauri na alipenda utani na kufurahi pale alipoona kila mtu anatabasamu na kufurahi.”
Hali ya majeruhi
Mmoja wa wanafamilia amesema mtoto wa marehemu aliyekuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, hali yake ya kiafya inaendelea kuimarika na tayari ameruhusiwa kutoka hospitali.
Maziko ya Padri Ngowi
Wakati huohuo, Paroko wa Parokia ya Mkula, Jimbo la Ifakara, mkoani Morogoro, Padri Nicolaus Ngowi aliyefariki dunia katika ajali ya gari juzi jioni atazikwa Jumatano ya Septemba 17, mwaka huu kwenye makaburi ya wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, yaliyopo Manyoni, mkoani Singida.
Padri Ngowi alifariki dunia papo hapo, Septemba 9, 2024 katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Kiruru Wilaya ya Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro.
Ajali hiyo ilitokea baada ya gari lake aina ya Toyota Prado alilokuwa akiliendesha kugongana uso kwa uso na basi la Kampuni ya Kilenga.
Padri Ngowi alikuwa akitokea Ifakara mkoani Morogoro akielekea nyumbani kwao Marangu Kilimanjaro kwa ajili ya kuhudhuria shughuli ya kifamilia iliyokuwa ifanyike Jumanne Septemba 10, 2024.
Akizungumza na Mwananchi leo jijini Dodoma, Mkuu wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, Tanzania, Vedasto Ngowi amesema maziko ya padri huyo yatafanyika Jumanne Septemba 17, mwaka huu Manyoni mkoani Singida.
Amesema kabla ya kuelekea Manyoni, Jumatatu Septemba 16, 2024 asubuhi kutakuwa na Ibada ya kumuombea marehemu itakayofanyika Parokia ya Makomu, Marangu mkoani Kilimanjaro.
Amesema ibada hiyo itaanza saa 6:00 mchana na baadaye wataanza safari ya kwenda Manyoni mkoani Singida.
“Jumanne, Septemba 17, misa ya mazishi itafanyika katika Parokia ya Manyoni kuanzia saa nne asubuhi. Baadaye maziko yatafanyika katika makaburi ya wamisionari wa shirika hilo,” amesema Vedasto.
Padri Ngowi alipata daraja la upadri mwaka 2004 na amefanya kazi zake za utume katika parokia za Boko, Kunduchi na Mtoni Mtongani za Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Pia, ametumikia Parokia za Itigi na Manyoni (Singida), Kondoa (Dodoma) na hadi umauti unamkuta alikuwa Paroko wa Parokia ya Mkula Jimbo Katoliki la Mahenge mkoani Morogoro.