Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira ataka somo la maadili lifundishwe kwa kila mwanafunzi

Muktasari:

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Stephen Wasira leo amewatunuku wahitimu 1,577 wa  ngazi mbalimbali kwenye mahafali ya 13 ya chuo hicho Kigamboni jijini Dar es Salaam

 Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Stephen Wasira amekitaka chuo hicho kuhakikisha somo la maadili na uzalendo linakuwa ni la lazima kwa kila mwanafunzi na liingizwe katika mitalaa.

Wasira alisema hayo leo wakati akizungumza katika mahafali ya 13 ya chuo hicho Kigamboni jijini Dar es Salaam na kuwatunuku wahitimu 1,577 wa ngazi mbalimbali.

"Nimefarijika kusikia chuo kimeanza kutoa mafunzo kwa vijana mbalimbali ya kuwajengea maadili ya uongozi,  uzalendo na utaifa, hivyo ni vyema kuhakikisha somo la maadili na uzalendo linakuwa ni la lazima kwa kila mwanafunzi na liingizwe katika mitalaa," alisema Wasira aliyewahi kuwa waziri kwenye tawala zilizopita.

Alisema hatua hiyo itasaidia  mwanafunzi kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu maadili na uzalendo wa nchi yake na taifa.

Miongoni mwa mafunzo waliyohitimu wahitimu hao ni ugavi na manunuzi, uchumi katika maendeleo, utawala katika biashara, uhasibu, uchumi, ualimu, Tehama na masuala ya jinsia na maendeleo.

Awali, akisoma taarifa ya chuo hicho, mkuu wa chuo hicho, Profesa Shadrack Mwakalila alisema idadi ya wahitimu imeongezeka katika mwaka wa masomo 2017/2018 na kufikia 1,577 ikilinganishwa na  mwaka 2016/2017 walikuwa  1,312.

Alisema udahili umeongezeka kutoka wanafunzi 5,173 mwaka 2016/2017 hadi kufikia wanafunzi 7,134 mwaka wa 2017/2018.

Alisema kati ya wanafunzi hao, 1,001 wamedahiliwa katika kampasi ya Zanzibar na 6,133 wamedahiliwa katika kampasi ya Kivukoni.

Kwa upande wake, waziri mkuu wa chuo hicho, Buhaga Obed alisema chuo hicho ni cha kipekee nchini ambacho ni mfano wa kuigwa kwa kuwa kinafuata nyayo zote za Mwalimu Julius Nyerere.

Aliwataka wazazi na walezi kuwaapeleka watoto wao katika chuo hicho kwa kuwa kinafundisha maadili na utawala bora hivyo kuwaandaa kujakuwa wananchi bora katika kulitumikia taifa.