Wastaafu EAC wakwama Mahakama ya AfcHPR

Wawakilishi na waliokuwa wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa kwenye Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu ( AFCHPR) kusikiliza hukumu ya kesi waliyofungua dhidi ya Serikali ya Tanzania juu ya malipo yao. Picha na Filbert Rweyemamu
Muktasari:
Kwa niaba ya jopo la majaji wenzake 10, Jaji Ore alisema maombi hayo hayatapokelewa hadi wahusika wafuate ngazi zote za ndani ya nchi.
Arusha. Jaji wa Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu (AfcHPR), Sylvian Ore kwa mara nyingine ametoa uamuzi wa kuyakataa maombi ya waliokuwa wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walioishtaki Serikali ya Tanzania.
Wanadaia kutolipwa mafao na kupigwa na polisi katika maandamano ya kudai haki ya kusikilizwa.
Kwa niaba ya jopo la majaji wenzake 10, Jaji Ore alisema maombi hayo hayatapokelewa hadi wahusika wafuate ngazi zote za ndani ya nchi.
Jaji Ore aliwataka wazee hao kufuata utaratibu wa Mahakama za ndani kutafuta haki zao kabla ya kukimbilia katika Mahakama hiyo inayojihusisha zaidi na kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu barani Afrika.
“Kwa kuwa walalamikaji hawajafuata utararibu unaotakiwa kabla ya kufikisha shauri mahakamani hapa, Mahakama hii inashindwa kupokea maombi yao kama yalivyowasilishwa, hivyo warudi kutafuta haki zao kwenye Mahakama za ndani ya nchi, wasiporidhika ndipo waje,” alisisitiza.
Hata hivyo, wazee hao waliilaumu Mahakama hiyo wakidai zipo njama zinazofanyika kati yake na Serikali ya Tanzania ili kuwanyima haki wanazodai tangu kuvunjika kwa EAC mwaka 1977.