Wataalamu kutoka Ufaransa watua Bukoba kukamilisha uchunguzi

Waokoaji wakiwatafuta manusura baada ya ndege ya Precision Air iliyokuwa imebeba watu 43 kutumbukia katika Ziwa Victoria Jumapili Novemba 6, 2022.Katika ajali hiyo 19 walifariki dunia huku 26 wakinusurika.
Muktasari:
Amesema ajali ya ndege ya Precision Air iliyosababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 24, inaendelea kufanyiwa uchunguzi na kwamba kikosi cha wataalamu kutoka Ufaransa kimekwenda kuchukua vitu muhimu kutoka kwenye ndege hiyo kwa ajili ya uchunguzi.
Bukoba. Mkuu wa mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amesema kampuni ya ATR ya Ufaransa iliyotengeneza ndege ya Precision Air iliyopata ajali Novemba 6, 2022 tayari wamewasili katika mkoa wa Kagera na wamechukua vifaa vinavyohitajika katika ndege kwa ajili ya uchunguzi.
Chalamila ameyasema hayo leo Novemba 12, 2022 wakati akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa ofisi yake kuhusu vipaumbele vya mkoa wa Kagera anavyotarajia kuvitekeleza wakati akiwa mkoani hapa.
Amesema ajali ya ndege iliyosababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 24, inaendelea kufanyiwa uchunguzi na kwamba kikosi cha wataalamu kutoka Ufaransa kimekwenda kuchukua vitu muhimu kutoka kwenye ndege hiyo kwa ajili ya uchunguzi.
“Swala la ajali ya ndege naweza kusema ni suala mtambuka, ni suala ambalo limekaribisha watu wengi. Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi inaendelea na kazi kuhusiana na maswala haya, nini hasa kimesababisha ajali hiyo na nini kinaweza kuja kufanyika baada ya matokeo ya uchunguzi wa ajali hiyo.
“Ajali inapotokea waliotengeneza ndege hizo huwa wanaamka haraka kutaka kujua ajali imetokanana na nini, hivi ninavyozungumza wenzetu Wafaransa ambao ndio wametengeneza ndege hiyo au injini hizo wameshafika katika mkoa wa Kagera na wamefungua vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya maswala ya uchunguzi,” amesema Chalamila.
Kuhusu chanzo cha ajali hiyo, Chalamila amesema tayari hatua za msingi zinaendelea na taarifa ya uchunguzi itakuwa chini ya Wizara na wao watautaarifu umma pale itakapofaa kuhusu chanzo sahihi cha ajali hiyo.
Amesema mkoa wake umeandaa andiko la mradi kwa ajili ya ujenzi mkubwa wa Uwanja wa Ndege wa Omukajunguti, wilaya ya Misenyi na kuipeleka wizara ya ujenzi na uchukuzi ambapo andiko hilo la mradi likipita utajengwa uwanja mkubwa.
Wakati huohuo, Chalamila amesema tayari kikundi cha wavuvi kilichopewa Sh10 milioni na serikali kimefungua akaunti katika benki ya CRDB na kuhifadhi fedha hizo na mdau mwingine, Azim Dewji kutoka kampuni ya usambazaji ya Simba ameunga mkono juhudi za serikali kwa kuchangia Sh10 milioni kwa kikundi hicho cha wavuvi