Wataalamu wa fedha nchini waaswa kuwa waadilifu
Muktasari:
Wataalamu wa Fedha na Mahesabu nchini wameaswa kuwa waadilifu wanapotekeleza majukumu yao na kuwa washauri wazuri kwa jamii katika kufafanua dira ya maendeleo ya uchumi nchini.
Arusha. Wataalamu wa Fedha na Mahesabu nchini wameaswa kuwa waadilifu wanapotekeleza majukumu yao na kuwa washauri wazuri kwa jamii katika kufafanua dira ya maendeleo ya uchumi nchini.
Hayo yamesemwa leo Novemba 12 jijini Arusha na Kamishna msaidizi idara ya uendelezaji wa sekta ya fedha wizara ya Fedha na Mipango, Janeth Hiza wakati akizungumza katika siku ya wahasibu duniani iliyofanyika katika chuo cha uhasibu Arusha .
Hiza amesema kuwa,wataalamu hao wanapaswa kuwa waadilifu na kutanguliza weledi katika utendaji kazi wao kwani idara hiyo ni muhimu sana kwa malachi ya nchi kwa ujumla.
Aidha amewataka wahasibu kuhakikisha wanajifunza udhibiti wa fedha haramu,pamoja na kuhakikisha wanajiunga na bima mbalimbali kwa ajili ya maendeleo yao .
"Nawaombeni sana mkajifunze kupata huduma jumuishi za fedha na mkatumie elimu zenu kufundisha jamii kuhusu elimu juu ya matumizi ya fedha na nidhamu ya fedha kwa ujumla kwani nyie ndio mnaotegemea katika jamii nzima inayowazunguka."amesema.
Kwa upande wake Naibu Mkuu wa chuo taaluma utafiti na ushauri wa kitaalamu Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Epaphra Manamba amewataka wahasibu hao kuhakikisha wanafanya kazi kulingana na sheria na taratibu zilizopo huku wakifuata maadili na matumizi sahihi ya fedha.
Profesa Manamba amewataka wanafunzi kufanya kazi kulingana na elimu na maadili waliyopata chuoni hapo ili wakawe mfano wa kuigwa katika jamii.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa idara ya fedha na uhasibu wa IAA, Dennis Hyera amesema kuwa siku ya wahasibu duniani kwa mara ya kwanza iliadhimishwa mwaka 1972 na wanajumuiya ya CPA wa San Diego Chapter katika taasisi ya Management Accountants .
Hyera amesema kuwa, siku ya wahasibu duniani imeanzishwa kwa ajili ya kuwahamasisha vijana walioko kwenye tasnia nzima ya uhasibu mnamo mwaka 1976 taasisi mbalimbali zilialikwa rasmi kusherehekea siku ya wahasibu duniani na ikarasimishwa kusherehekewa mahali popote na nchi yoyote kila ifikapo Novemba 10 kila mwaka .
Makamu wa Rais Serikali ya Wanafunzi (IAASO), Shazma Edward amesema kuwa kupitia siku ya wahasibu duniani wamejifunza mambo mengi ikiwemo kutanguliza maadili na uzalendo katika utendaji kazi wao wa kila siku ili taaluma hiyo iendelee kuboreka zaidi.