Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wataalamu wafichua usichokijua madai ya bima

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), madai ya bima yanapaswa kulipwa ndani ya siku 45 baada ya mteja kusaini fomu ya makubaliano (discharge voucher).

Dar es Salaam. Wataalamu wa bima wamewataka Watanzania kuondoa dhana potofu kuwa madai ya bima ni msaada wa hiari kutoka kwa kampuni za bima, wakisisitiza kwamba ni wajibu wa kisheria unaotokana na mkataba kati ya mteja na mtoa huduma.

Akizungumza katika mkutano wa mtandaoni (webinar) ulioandaliwa na Stanbic Bank Tanzania, Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Callinggod Temu amesema mara mtu anapolipia bima, kampuni inalazimika kisheria kumlipa iwapo tukio lililokatiwa bima litatokea.

“Madai ya bima si malalamiko ni wajibu wa kisheria wa mkataba. Wamiliki wa bima wanapaswa kuelewa hili na kusoma mikataba yao kabla matatizo hayajatokea,” amesema.

Aidha, Ofisa Mauzo wa Bima wa Stanbic Bank, Naphtal Ntangeki amesema changamoto nyingi zinazojitokeza hutokana na wananchi kutozingatia taratibu za msingi, ikiwemo kutoa taarifa kwa wakati na kuwasilisha nyaraka sahihi.

Kwa upande wake, Suzane Nyangi kutoka Metropolitan Insurance ameeleza kuwa migogoro mingi ya madai inaweza kuepukika endapo wateja wataelewa vipengele vilivyoachwa kwenye sera na kuzingatia masharti.

Meneja Mwandamizi wa Bima wa Stanbic Bank, Jumanne Mbepo, amesema watoa huduma nao wana wajibu wa kutoa elimu.

“Kabla ya majanga kutokea, lazima tuwafundishe wateja haki na wajibu wao. Dai la bima ni haki, siyo upendeleo,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), madai ya bima yanapaswa kulipwa ndani ya siku 45 baada ya mteja kusaini fomu ya makubaliano (discharge voucher).

Stanbic Bank imekuwa ikitumia mkakati wa benki bima (bancassurance) kupeleka elimu na huduma za bima karibu na wananchi, hatua inayolenga kuongeza uelewa na kupunguza migogoro ya madai.