Wataalamu wagundua mashine ya kuzalisha taulo za kike kwa Sh200

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akisikiliza maelezo ya utendaji kazi wa mashine ya kununua Pedi kwa njia ya Shilingi (Vending machine) kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Bela Vendor Tanzania, Lulu Ameir katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge iliyopo mkoani Dodoma.

What you need to know:

  • Kutokana na tafiti kuonesha wanafunzi wengi wanakosa masomo siku 30 hadi 40 kwa mwaka wanapokuwa kwenye siku za hedhi, wataalamu wamebuni mashine itakayomwezesha mwanafunzi kununua pisi moja ya pedi kwa Sh200.

Dodoma. Serikali imezindua mashine itakayomwezesha mwanafunzi kununua pisi moja ya taulo ya kike kwa Sh200 ili kusaidia wanafunzi wanaokosa masomo kutokana na ukosefu wa miundombinu rafiki ya kujihifadhi wakati wa hedhi.

Hata hivyo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewaagiza wataalamu wa mashine hiyo na watendaji wake kufika ofisini kwake kujadili ni utaratibu upi utatumika kufunga mashine hiyo katika shule mbalimbali nchini.

Mashine hiyo imezinduliwa leo Mei 26, 2023 na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Bunge kueleka siku ya hedhi salama duniani inayoadhimishwa Mei 27 kila mwaka.

Ummy amesema mashine hiyo itasaidia wanafunzi wa kike wanaokadiriwa kukosa masomo kwa siku 30 hadi 40 ambazo hutega shule kwa kukosa mazingira rafiki ya kujihifadhi wakati wa hedhi ikiwemo ukosefu wa taulo.

Akizungumzia utendaji kazi wa mashine hiyo ambayo haitumii umeme kujiendesha, Mtendaji mkuu wa Taasisi ya Bela, Vendor Tanzania Lulu Ameir amesema wazo la kutengeneza mashine hiyo lilikuja kutokana na baadhi ya wanafunzi kuathiri mwenendo wa elimu yao kutokana na kutohudhuria masomo katika siku zao za hedhi.

Lulu amesema mashine hiyo huwekwa Sh200 na kuruhusu kutoa pisi moja ya pedi ambayo itamsaidia mwanafunzi kujihifadhi na kuendelea kusoma badala ya kurudi nyumbani.

Blandina Morris ni mwanafunzi wa kidato cha sita Shule ya Sekondari Bunge ambaye anasema awali baadhi ya wanafunzi ambao walishindwa kununua taulo hizo walipata changamoto hivyo kuwaomba walimu wao wawanunulie.

“Tulikuwa tunawasumbua walimu kama mwanafunzi atakosa sh2,000 ya kununulia pedi lakini kwa Sh200 naamini kila mmoja wetu ataweza kumudu kujinunulia mwenyewe wakati wowote," amesema Blandina.